Friday, May 24

ON OUR UNION: FARRELL CALLS A SPADE A SPADE, NOT A GARDENING TOOL!

0


Farrell
Anaandika Farrell Jnr:

#ZanID


Moja ya kitambulisho kilichotumia fedha nyingi za umma kuhakikisha wakaazi visiwani wanamfumo wa utambulisho utaorahisisha maisha. Tumemsikia majuzi mmoja wa wawakilishi akisema kwamba mfumo uliotumika katika ZanID umetambulika na kupewa tunzo kwa uthabit wake. Katika nchi ya watu milioni moja na ushee kuwa na mfumo wa utambulisho wa namna hii ni ishara ya utayari wa kuenda na wakati hasa huu wa dunia ya sasa ya teknolojia.


#NIDA


Kwa wananchi milioni moja visiwani sioni hasa sababu ya kuwa na vitambulisho viwili. Nafikiri gharama iliotumika kwa ZanID ingetosha kuwa kielelezo cha kupunguza gharama na istifham ya vitambulisho viwili ambavyo kiukweli havina tafauti yeyote zaidi ya jina la taasisi inayovitoa. Mathalan waskochi, wao wanapesa tafauti kabisa na paund ya Muingereza lakini paundi ya mskochi inatumika kila pembe ya Himaya nzima ya Muungano wa kifalme (UK), hizi ni jitihada za Bank of England na serikali kuu kuona thamani ya utambulisho wa Scotland, historia yake katika kujitawala na zaidi hisia za wananchi wa Scotland kwa nchi yao ndani ya Muungano huu wa Himaya ya kifalme.


#Istifham


Sasa unajiuliza ikiwa pesa ya mskochi inatumika pande zote za Muingereza iweje basi kwetu lazima tuwe na vitambulisho viwili vinavyobeba gharama isiohitajika? Tunanadi vipi kupunguza gharama wakati tunashindwa na madogo ya kitambulisho tu wakati wenzetu mkabala nasi wamefika hatua ya kutoa fedha za kwao wenyewe kukuza utambulisho wa kihistoria wa mamlaka zao. 


#Kero


Na si ZanID tu lakini mtiririko wa mambo mengi yanayofanya kulazimisha ile ashki ya kuidogosha Zanzibar na mamlaka yake. Umepata kumuona Rais wa Zanzibar anavyopokelewa anapokuwa upande wa pili wa Muungano? Sikuwahi kushuhudia hata mkuu wa Mkoa akimpokea wakati kwetu huku mpaka chekechea hupangwa mstari kumpokea Waziri tu seuze Rais. Na halkadhalika kwa gari zenye namba za Zanzibar, unaweza kuzikuta za Burundi lakini ya Zanzibar marufuku. Kila kinachobeba utambulisho wa Zanzibar hata kiwe na ubora wa aina gani kwa upande wa pili kitadhalilishwa, kudogoshwa na kudhoofisha kisiwe na thamani. 


Tusiende mbali, maziwa ya Bakhresa yanayozalishwa visiwani yalizuiwa kwa muda kwa vijisababu mpaka alipokubali kuwekeza kiwanda kama cha Zanzibar cha maziwa upande wa pili. Hebu funga macho ujiulize lengo ni lipi? Sakata la VAT, mafuta na gesi zinazoagizwa nje, na mengi yanayotugharimu na kuyafanya maisha kuwa magumu zaidi kwa wazanzibari ni sehemu ya “mindset” hizi zinazozaa kero.


#SpikaAjabu


Bungeni suala la Zanzibar kama kawaida limebebwa na tashtiti za Spika Ndugai alieona ni upuuzi kuwaambia wageni kuwa Tanzania ni taifa la nchi mbili. Anasema hao wageni watatufahamu vipi? Sitatumia neno dhaifu maana bwana mkubwa halitaki kulisikia lakini nashindwa kupata mbadala wa neno atalolifurahia. 


Spika huyu ameshawahi kuwa kiongozi wa maspika wa Jumuia ya Madola, hivi atapoambiwa Himaya ya Muingereza inajengwa na mamlaka mbali ya House of Common na Lords lakini pia na Bunge la Waskochi (Holyrood), Senedd la wa Welsh na lile la wairish wa Kaskazini (Stormont) hatawafahamu? 


Hivi kweli hatawafahamu Hongkong na mfumo wake wa kiutawala ndani ya China? Ikiwa wageni watashangazwa na neno nchi mbili, jee nae atamtambulisha vipi Rais wa Zanzibar bila ya mshangao? Hivi anapomualika bungeni Rais wa Zanzibar hajishangai mwenyewe kumualika Rais asie na nchi kwa tafsiri ya Zanzibar kuwa si nchi? 


#BungeVBLW


Waziri Zanzibar katika BLW anasema kuwa ZanID haitumiki kwa sababu ya mifumo tu tafauti na ya NIDA. Utashangaa iweje chama hichi hichi chenye uongozi pande zote mbili na sera sawa zisishindwe kutazama mapema mfumo bora utaobeba pia ZanID ilioanza kufanya kazi takriban miaka mitatu kabla ya NIDA?


Kubwa zaidi ni jinsi majibu ya Waziri upande wa pili katika suala mfanano na hili anasema nchi ni moja tu na mamlaka ya vitambulisho viko upande mmoja na si suala tena la kinachoitwa “Mfumo Tafauti”. Tuseme Waziri alilidanganya BLW kwa majibu yake hasa kwa kuzingatia majibu ya upande wa pili?


#Katiba


Katiba ya Zanzibar inatamka wazi kuwa ni nchi, na tamko hili lipo mwanzo kabisa katika utambulisho wake. Na Katiba ya Muungano ina sehemu maalum inayoeleza mamlaka ya Zanzibar, Rais wa Zanzibar, Mahakama Kuu Zanzibar, Baraza la Wawakilishi na Katiba ya Zanzibar. Chama cha Mapinduzi kinaongoza nchi kwa misingi ya Katiba hizi mbili, sasa kwa nini hakufunguliwi mahakama ya Kikatiba kama ambavyo Katiba ya Muungano inavyojieleza ili kupata suluhu ya kudumu katika hili suala la Zanzibar kuwa nchi au si nchi badala ya kejeli za kitoto zinazobeba maudhi kwa wengine? Na zaidi hasa mahakama hio ieleze basi kama Zanzibar si nchi ni kitu gani, Mkoa au shehia au kitongoji katika Jamhuri ya Muungano?


#Udhaifu


Ninaamini kuwa sababu kubwa ya watawala Zanzibar kushindwa chaguzi ni haya matamshi ya kidhalili dhidi ya Zanzibar. Na kila panapokosekana weledi wa matamshi haya ndio huzidi kubeba changamoto kwa watawala Zanzibar kwa sababu ni wachache miongoni mwa wazanzibari watakaopanga foleni ya kupiga kura kuwapa wanaokubali udhalilishaji wa aina hii na matamshi holela. 


Ikiwa CCM inatafuta hasa tatizo la anguko lake basi ni hili la Muungano na kauli za Kilukuvi. Kibri hichi kinaweza kustahamiliwa na watawala wanaotegemea “nguvu” kufuta chaguzi, tab’an ni ari ya wananchi tokea 1995 inayowafanya watawala Zanzibar kuwa na wakati mgumu kila chaguzi na kupoteza mvuto hata katika sehemu zinazotambulika kubeba wafuasi wake wengi.


#Ajabu


a) Siamini kama ZanID haiwezi kuwa “integrated” katika NIDA, ikiwa tunajenga mfumo wa pasi za usafiri wa Jumuia ya Afrika Mashariki tushindwe vipi na kijisehem cha ZanID za watu milioni moja? Ikiwa Bara hakikubaliwi kitakubalika wapi pengine? Taifa  moja la Muungano lisilokubali kitambulisho cha mdau mmoja kweli inayumkinika?


b) Si kweli kuwa hii nchi moja, katiba ya Zanzibar inatamka wazi kuwa ni nchi katika Taifa la Muungano wa Tanzania. Kwa nini jitihada kubwa zinatumika kufuta uwepo wa Zanzibar kama nchi badala ya kuukabili ukweli wa nchi mbili katika taifa moja lililoungana ukizangatia katiba ya Zanzibar, mabadiliko yake ya 2010 na uungwaji mkono kwa asilimia zaidi ya 60 ya wananchi? 


c) Si kweli kuwa wageni watatushangaa kwa kejeli za kuwa nchi mbili ndani ya taifa la Muungano wa Tanzania, hawajaishangaa HongKong ambayo si nchi lakini ikabeba mamlaka kiasi kwamba mchina kutembea HongKong bila kibali hawezi. Hawaishangai Gibraltar, inayoshiriki hata World Cup ikiwa ni sehemu ya Himaya ya Muingereza, hawaishangai Scotland ilio na First Minister wake mwenye hadhi kamili ya mtawala anaeongoza serikali na bunge ikafika hadi akaitisha kura ya maoni kujitenga na Himaya ya kifalme. 


d) Hivi huko nyuma tulipotembelewa na kina Che Guevara, Haile Selasie, Gamal Abdel Naser, Mandela, Prince Charles, Joachim Gauck wote hawa hawakushangaa mpaka wakapigiwa mizinga 21 kwa heshima ya nchi yenye historia kubwa wakati tupo katika muungano?


#Stahili


Kwa hili huwacheka zaidi wale wale waliokabidhiwa “Blue Print” ya dhahabu na Mzee Warioba wakaghilbika na kugeuka samaki kwa usahaulifu mwisho wake wakamtusi, kumdhihaki na kuichezea ngoma kilichoitwa mbadala “Rasimu ya Mzee Sita”. Yanayowafika mkiwa bungeni ni kile kile alichokitanabahisha Dr Karume kuwa ni usamaki na usahaulifu wa kujitakia. Matokeo Bara munapozungumza haya ya msingi munaonekana kero na visiwani munabaki kuwa gumzo la vijiweni.


#Nasaha


1. Wakati umefika wa kujitangaza wenyewe na mamlaka yetu tulionayo. Huwezi kutegemea “Goodwill” ya anaeonekana wazi wazi akipinga jitihada za kuboresha uchumi na maelewano na wengine yenye tija kwa sababu za ajabu kama hii ya “dunia kushangaa nchi mbili katika Muungano”. Tujitangaze kama katiba yetu inavyotamka, na kuainisha mamlaka tulio nayo, gharama zetu za kuendesha serikali na jitihada za kujikomboa katika umasikini. 


2. Wakati wa kutazama uwezekano wa kujiimarisha wenyewe kwa kuwa na meza maalum katika nchi mashuhuri zitazosimamia ukuaji wa utalii na kujitangaza ikiwamo mialiko maalum ya viongozi watakaoinua jina la Zanzibar. Hili linawezekana ikiwa nia thabit ipo. Wako viongozi mashuhuri watakaobeba “Ulezi” kwa Zanzibar na kuhuisha jina litakalozidisha utalii na kuongeza pato la nchi.


3. Na kwa hili la ZanID halkdhalika tuna historia kubwa na nchi tafauti duniani ambazo zina balozi ndogo Zanzibar ambazo tunaweza kuwafikiana matumizi ya ziada ya ZanID katika mahusiano yatayokifanya kitambulike na kuheshimika pamoja na kubeba faida kwa wakaazi wetu wanapokuwa katika sehemu husika. Ikiwa kitambulisho cha mwanafunzi kina thamani katika taasisi tafauti duniani, tushindwe vipi kuwa na makubaliano ya tija kwengine kwa matumizi ya ZanID? Tunachohitaji ni muamko, jitihada na utayari wa kuhakikisha fedha zilizotumika katika ZanID zinabeba faida kwa wananchi na nchi kwa jumla.


As received

Share. Twitter Facebook Google+ Pinterest LinkedIn Tumblr Email

About Author

Leave A Reply