Friday, March 22

Maalim: ”Kwa lugha ya CCM, bado muda haujafika”!

0


Maalim Seif

Katibu mkuu wa chama cha Wananchi, CUF Maalim Seif amesema kwa mujibu wa lugha ya CCM muda wa kutangaza nia kama 2020 atawania Urais bado haujafika huku pia akiweka wazi kuwa muswada wa sheria mpya ya vyama vya siasa, unaeleza hofu iliyonayo CCM.


”Bado mbali, muda wa kutangaza nia haujafika kwa mujibu wa lugha ya CCM”, ameeleza Maalim alipoulizwa endapo ana mpango wa kugombea mwaka 2020.

Maalim Seif pia ameeleza kuwa, uwepo wa kifungu kinachomzuia mtu kugombea nafasi yoyote ya kisiasa ndani ya mwaka mmoja anapokuwa amehamia chama kingine ni dhahiri kuwa CCM, inahofu juu ya wabunge au viongozi itakaowatema 2020.


”Muswada ukipita unasema mtu aliyeacha chama chake hatoruhusiwa kugombea katika chama chochote mpaka mwaka mmoja upite labda kuna hofu CCM ikawatema wabunge wake mwaka 2020 na wasiruhusiwe kugombea katika vyama vya upinzani”, amesema Maalim.

Aidha Maalim Seif ameweka wazi hofu yake nyingine juu ya muswada huo ni kipengele kinachomtaka Waziri mwenye dhamana ndio atoe ruhusa ya vyama kuungana kitu ambacho kitakuwa kigumu kwani waziri anakuwa anatoka chama tawala ambacho kinakuwa kinaunda serikali.

Muswada huo wa Sheria mpya ya vyama vya Siasa ulijadiliwa bungeni kwa mara ya kwanza katika mkutano wa 13 wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kilichoaanza Novemba 6 na kumalizika Novemba 16, 2018.

Share. Twitter Facebook Google+ Pinterest LinkedIn Tumblr Email

About Author

Leave A Reply