Sunday, May 26

*ANAANDIKA HON. TUNDU LISSU KUTOKA BELGIUM*!

0


Huwa sina tabia ya kujibizana hadharani na Mheshimiwa Mwigulu Nchemba kwa sababu, tofauti na wengi wengine, ninafahamu na kuheshimu msimamo wake, japo wa mafichoni. 

Kwenye hili la wasimamizi wa uchaguzi, hata hivyo, naomba kutofautiana naye hadharani.

Suala la wasimamizi wa uchaguzi kutokuwa wanachama wa vyama vya siasa sio suala ‘mufilisi’ kabisa. Suala hili ni amri ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977. 

Ibara ya 74(14) ya Katiba hiyo inaamrisha kwamba “itakuwa ni marufuku kwa watu wanaohusika na uchaguzi kujiunga na chama chochote cha siasa….” 

Katiba imewataja watu hao ‘wanaohusika na uchaguzi’ kuwa ni pamoja na “wasimamizi wote wa uchaguzi wa miji na Wilaya zote.” (Ibara ya 74(15)(e).

Kwa Sheria ya Uchaguzi, 1985, wakurugenzi wote wa majiji, miji na wilaya ndio wasimamizi wa uchaguzi katika nchi yetu. Katika masuala ya uchaguzi, haki pekee waliyo nayo watu hao, kwa mujibu wa ibara ya 74(14), ni haki ya kupiga kura tu.

Wasimamizi wa uchaguzi hawa ni maafisa wa Tume ya Uchaguzi sio kwa kuteuliwa, bali by operation of the law. Wamelazimishiwa Tume, sio kwa mapenzi ya Tume, bali kwa shuruti ya Sheria ya Uchaguzi. 

Hata hivyo, bado wanabanwa na amri ya ibara ya 74(14) na (15) ya Katiba. Ni marufuku kuwa wanachama wa chama chochote cha siasa. 

Isingekuwa tuko kwenye Tanzania ya Magufuli ningeona ajabu kwamba mtu ambaye, kama Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, amewahi kushikilia madaraka makubwa kama ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, anaweza kuwa kwenye giza nene kiasi hiki juu ya matakwa ya Katiba ya nchi yetu. 

Lakini tuko kwenye Tanzania ya Magufuli ambayo kwayo Katiba na Sheria za nchi ni makaratasi tu. Kwa Tanzania hii, Katiba na Sheria halisi ni kauli na matamko yanayotoka kwenye kinywa cha mtukufu Rais. 

Na kwa sababu hii tu, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba ni mtu wa kusamehewa, kama sio wa kuonewa huruma, kwa sababu na yeye pia ni mhanga wa Tanzania ya Magufuli. 

Hoja ndogo ya mwisho kuhusu suala hili. Sio tu kwamba Rais Magufuli amekiuka Katiba na Sheria ya Uchaguzi kujaza makada wa CCM kwenye uongozi wa Halmashauri za Serikali za Mitaa, bali pia katika kufanya hivyo, Rais amenyakua madaraka yasiyokuwa yake. 

Sheria yetu ya Utumishi wa Umma imeweka wazi utaratibu na mamlaka ya kuteua wakurugenzi wa Halmashauri hizo. Mamlaka hayo ni ya Tume Kuu ya Utumishi wa Umma, kwa kupitia Tume ya Utumishi wa Serikali za Mitaa. 

Na wanaotakiwa kuteuliwa kuwa wakurugenzi wa Halmashauri hizo ni watu walioko kwenye utumishi wa umma, sio makada wa CCM waliokosa ubunge. Kama hili nalo halieleweki kwa akina Mwigulu Nchemba basi tuna tatizo kubwa kuliko tunavyofikiri. 

Wasalaam
TL
Share.

About Author

Leave A Reply