Thursday, February 21

Paul Makonda Alivyokumbana na Vikwazo Vingi Kutokana na Matamko yake

0


Licha ya kutikisa katika utendaji wake tangu alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amejikuta akikumbana na vikwazo katika maagizo na matamko yake ambayo mara kadhaa yametofautiana na mtazamo wa viongozi wenzake serikalini.

Mkuu huyo wa mkoa ambaye aliteuliwa kushika wadhifa huo akitokea kwenye nafasi ya ukuu wa Wilaya ya Kinondoni, Machi 2016, miezi michache kabla hajamteua, Rais Magufuli akizungumza na wazee wa Dar es Salaam alieleza kuridhishwa na utendaji wake wa kazi.

Rais alifikia hatua hiyo ya kumpongeza na kumsifia kutokana na utendaji wake katika wilaya hiyo hasa katika elimu.

Baada ya kupandishiwa cheo, mkuu huyo wa mkoa alitangaza vipaumbele vyake na kuahidi kuvifanyia kazi. Baadhi ni pamoja na upatikanaji wa madawati, vyumba vya madarasa, usafi wa mazingira, kuboresha Soko la Kariakoo, kero ya wamachinga katikati ya jiji, ombaomba na usafiri.

Hata hivyo, nyingi ya ahadi hizo sio tu kwamba zimeishia hewani, bali zimemuingiza kwenye misukosuko au kupingana na mtazamo wa viongozi wenzake serikalini.

Februari 2017, Makonda alianzisha vita dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya akiwataja baadhi ya maofisa wa Jeshi la Polisi aliodai kuwa wanashirikiana na wasanii wanaojihusisha na uuzwaji na utumiaji wa dawa hizo.

Kama hiyo haitoshi, Februari 8, alitaja majina 65 na kampuni tatu akidai kuhusika na matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

Miongoni mwa walioguswa ni na wafanyabiashara, wanasiasa na viongozi wa dini akiwamo Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.

Wakati Makonda akiendelea na kampeni hiyo, Rais Magufuli alimteua kamishna mpya wa mamlaka ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya, Rodgers Sianga,

Ili kukamilisha vita yake ya dawa za kulevya, Februari 13 alikabidhi majina 97 ya watuhumiwa dawa za kulevya kwa Kamishna Mkuu wa Tume ya Kudhibiti na Kuzuia Dawa za Kulevya, Sianga ili ayashughulike.

Wakati mpambano huo ukiendelea huku akichuana na Askofu Gwajima, Makonda alishiriki ibada ya maombezi katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kimara, alikoangua kilio alipokuwa akiombewa.

Kabla tukio hilo halijafutika machoni na masikioni mwa watu, mkuu huyo wa mkoa alidaiwa kuvamia kituo cha Redio cha Clouds Media Mikocheni Dar es Salaam akiwa na watu waliobeba silaha akidaiwa kuwalazimisha watangazaji wa kipindi cha Shilawadu kutoa habari iliyomhusu mwanamke aliyedaiwa kutelekezwa na Askofu Gwajima.

Uvamizi huo uliorekodiwa na kamera za usalama (CCTV) za kituo hicho, ulisababisha aliyekuwa Waziri wa Habari, Nape Nnauye kuunda kamati ya kuchunguza tukio hilo.

Lakini Makonda hakutoa ushirikiano kwa kamati hiyo. Siku chache baadaye, Nape alitenguliwa uwaziri.

Jambo jingine aliloanzisha Makonda ni kuwasaka wanaume waliotelekeza wanawake na watoto, aliwaita ofisini kwake akiwataka wawataje wenzi wao waliowatelekeza.

Suala hili liliingiliwa kati na Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile aliyesema suala hilo linapaswa kushughulikiwa na Wizara ya Afya, kitengo cha ustawi wa jamii.

Kazi hiyo iliyodumu kwa siku tano, ilihitimishwa kwa Makonda kuwatangazia kinamama wote waliofika ofisini kwake wakiwa na watoto atawapatia kadi za Bima ya Afya (Toto Afya Card) bure kwa ajili ya matibabu ya watoto wao.

Alisema kadi hizo zitatolewa kwa watoto wenye umri chini ya miaka 17 kwa kila mama aliyefika ofisini kwake pasipokujali idadi ya watoto alionao.

Kikwazo kingine alichokikwepa Makonda ni makontena yake 20 yaliyokwama katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kushindwa kulipiwa kodi.

Sakata la makontena hayo lilianza baada ya tangazo la TRA lililochapishwa kwenye gazeti la Serikali la Daily News Mei 12, likiwataka wamiliki wa mali zilizokaa bandarini kwa zaidi ya siku 90 kujitokeza kuzilipia.

Tangazo hilo lililokuwa na orodha ya makontena zaidi ya 800, jina la Paul Makonda lilijitokeza mara 20 akiwa mpokeaji idadi hiyo ya makontena yaliyokuwapo katika bandari kavu ya DICD yakiwa na samani.

Jitihada za Makonda kuyaomba msamaha makontena Wizara ya fedha zilishindikana baada ya Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango kumkatalia. Kama hiyo haitoshi Dk Mpango alisisitiza kuyapiga mnada makontena hayo akipinga kauli ya Makonda kuwa atakayeyanunua atalaaniwa.

Mbali na Waziri Mpango, Rais Magufuli akizungumza na madiwani, viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Geita Agosti 30 aliagiza kupigwa mnada kwa makontena hayo.

Hivi karibuni RC Makonda amewataka wakazi wa Dar es Salaam kuwataja watu wanaojihusisha na vitendo vya ushoga huku akisema kabla ya jana wenye simu za ngono kwenye simu zao wawe wamezifuta.

Hatua ya Makonda ilikuja baada ya kusambaa kwa picha za utupu za mwanamke anayeitwa Amber Rutty na za msanii wa filamu wa Bongo Movie Wema Sepetu katika mitandao ya jamii.

Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje juzi jioni ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikimkana Makonda na kwamba kampeni ya kuwasaka watu wanaojihusisha na vitendo vya ushoga inayoratibiwa naye ni mawazo yake na si msimamo wa Serikali.

“Serikali ya Tanzania ingependa kufafanua kwamba hayo ni mawazo yake (Makonda) na si msimamo wa Serikali,” ilisema taarifa ya wizara hiyo kwa vyombo vya habari.

Maoni ya wadau

Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob alisema mambo yanayotekelezwa na Makonda hayajawahi kujadiliwa kwenye Baraza la Jiji wala Baraza la Ushauri wa Mkoa. “Tunakutana mara mbili kwa mwaka, hajawahi kuleta jambo lolote kwa ajili ya kujadili, yote ni mambo yake mwenyewe,” alisema Jacob.

Alisema Mkoa wa Dar es Salaam una kamati ya mambo ya jamii inayohusika na mambo kama dawa za kulevya, ushoga na ndoa za jinsia moja, lakini hajawahi hata kufikisha masuala hayo kwenye kamati hizo.

Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara amemtetea Makonda akisema anatekeleza majukumu yake hata kama hayafiki mwisho. “Kazi ya Mkuu wa Mkoa ni pamoja na kusimamia miradi ya maendeleo ya mkoa wake pamoja na ulinzi na usalama,” alisema Waitara.

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita alisita kuzungumzia akisema yuko kwenye kikao.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Anna Henga alisema bado wanayatafakari mambo hayo kwenye vikao vya ndani likiwemo suala la ushoga hadi watakapotoa tamko rasmi.

By Elias Msuya, Mwananchi emsuya@mwananchi.co.tz

Install Application ya Udaku Special Uweze Pata Habari Kama Hizi Kirahisi Zaidi
=>BOFYA HAPA KUINSTALL/DOWNLOAD

Share.

About Author

Leave A Reply