Monday, August 26

Afisa Elimu, Polisi Wavunja Ndoa ya Mwanafunzi

0


Afisa elimu, polisi wavunja ndoa ya mwanafunzi

Afisa elimu Sekondari Wilaya ya Geita, Richard Mwakibinga kwa kushirikiana na askari polisi wa kituo kidogo cha Rwamgasa wilayani humo, wamefanikiwa kusambaratisha ndoa ya mwanafunzi.

Mwanafunzi, Sundi Malongo (16) anayesoma  kidato cha nne katika shule ya Sekondari Rwamgasa, alitakiwa kuozeshwa kwa mahali ya ng’ombe sita na mbuzi watatu.

Tukio hilo limetokea majira asubuhi wakati mshenga wa muoaji na kaka wa muoaji walipofika shuleni hapo kumuombea ruhusa mwanafunzi huyo wakidanganya ni mgonjwa na anakwenda kutibiwa huku wakijifanya ni ndugu wa mwanafunzi wakati lengo ni kumtoa mazingira ya shule na kwenda kumkabidhi kwa mumewe aliyefahamika kwa jina la Paulo Nderea Makeregesha.

Kwa vile mwanafunzi huyo alishatoa taarifa shuleni kila hatua kuhusu ndoa yake hiyo, ikamlazimu mkuu wa shule hiyo Masaguda Kamena kuwasiliana kwa siri na Afisa Elimu Sekondari Richard Mwakibinga akimtaarifu ujio wa waoaji hao shuleni.

Afisa Elimu Mwakibinga aliwasili shuleni hapo akiwa na askari polisi wa kituo cha Rwamgasa kisha kuwatia mbaroni mshenga, kaka wa muoaji, na mzazi wa muolewaji, Isheli Makeregesha.

Hawakuishia hapo, wakaondoka kwao na wazazi wa mwanafunzi huyo na kukuta shamrashamra zikiendelea na kufanikiwa kumtia mbaroni mzazi wa mwanafunzi huo Kwiyema Malongo.

Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo, mipango ya kutaka kuozwa kwa mwanamume huyo, mkazi wa kijiji cha Shilungule Kata ya Busanda ilianza akiwa darasa la saba.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo hakupatikana kuzungumzia sakata hilo na juhudi za kumtafuta zinaendelea, huku baadhi ya wanafunzi wakilaani vikali tukio hilo.

Share.

About Author

Leave A Reply