Monday, August 26

POLISI WAUA WATU 4 WANAODAIWA KUWA MAJAMBAZI KATIKA MAJIBIZANO YA RISASI

0


Watu wanne wanaodaiwa kuwa ni majambazi, wameuawa na polisi wakati wakiwa kwenye majibizano ya risasi ndani ya msitu wa Kisanga Kijiji cha Kisanga Tarafa ya Mikumi wilayani Kilosa mkoani Morogoro huku wengine 19 wakishikiliwa.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Wilbrod Mutafungwa alisema kuwa tukio hilo ni Mei 16 mwaka huu majira ya saa tisa alasiri katika pori hilo lililipo Kijiji cha Kisanga wilaya ya kipolisi ya Ruhembe.

Kwa mujibu wa kamanda huyo, polisi wakiwa wanafuatilia matukio ya mauaji na unyang’anyi wa kutumia silaha yaliyokuwa yamefanyika katika maeneo tofauti ya tarafa za Mang’ula na Ifakara wilaya ya Kilombero, walipata taarifa kuwa watuhumiwa waliojihusisha na matukio hayo, walikimbilia kwenye pori lililo karibu na Kijiji cha Kasanga kujificha ili wasikamatwe.

Kwamba baada ya kupata taarifa zao, polisi waliwafuata na kukuta kundi la watuhumiwa hao, lakini wao baada ya kuwaona askari, walielekea walipo na kuanza kuwavyatulia risasi. 

Kufuatia shambulizi hilo, askari walilazimika kujibu mashambulizi hayo, huku wakiwa kwenye tahadhari wasidhuriwe.

Hata hivyo katika majibizano hayo, watuhumiwa wanne walijeruhiwa kwa risasi sehemu mbalimbali za miili yao. Wengine walitokomea porini na hawakupatikana. 

Kamanda Mutafungwa alisema watu hao wanne walikufa, baada ya kuvuja damu nyingi wakiwa njiani kupelekwa hospitalini kupatiwa matibabu.

Alisema watu hao walikutwa na bunduki mmoja aina ya shortgun double barrow yenye namba 107735, iliyokatwa kitako na mtutu ikiwa na risasi mbili na ganda moja la risasi. Kwamba watu hao walihusika kwenye matukio mbalimbali ya uporaji na ujambazi katika tarafa ya Mang’ula.

Mbali na kuuawa kwa watuhumiwa hao wa ujambazi, Polisi waliendesha msako na kufanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa wengine 19, wakiwemo wapangaji wa matukio hayo ya ujambazi, ambao ni wakazi wa miji ya Ifakara, Man’gula, Kiberege na Ruaha.

Mutafungwa alisema watuhumiwa wote wanaoendelea kuhojiwa na upelelezi utakapokamilika, watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili. 

Miili ya waliouawa imehifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.

Share.

About Author

Leave A Reply