Sunday, August 18

KAHAMA WAKUMBWA NA MAFURIKO MAKUBWA

0


Baadhi ya wakazi wilayani Kahama mkoani wa Shinyanga wamekumbwa na mafuriko kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha na baadhi yao kuokolewa na Jeshi la Zimamoto na kupelekwa maeneo salama.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, mkuu wa wilaya ya Kahama, Annamringi Macha alisema hali ni mbaya karibu mji mzima. “Hivi sasa tuko maeneo yaliyozingirwa na maji kwa ajili ya kufanya tathmini ya athari, nitatoa taarifa rasmi baada ya kumaliza kazi hii,” alisema.

Nyumba zilizoathiriwa zaidi na mafuriko hayo ni zilizojengwa maeneo ya mabondeni katika kata za Mhongolo, Majengo, Nyihogo, Nyasubina na Mwanva.

“Lakini hata maeneo mengine ya vijijini tuna taarifa kuwa nako mvua imenyesha na imeathiri baadhi ya sehemu,” alisema. Macha.

Mmoja wa waathirika wa mafuriko hayo, Elizabeth Peter mkazi wa mtaa wa Mhongolo alisema mvua hiyo iliyonyesha kuanzia saa 3:00 usiku juzi hadi saa saba usiku wa kuamkia jana imesomba vyombo vyote vya ndani na vyakula katika nyumba yake.

Alisema kwamba nyumba nyingi katika kata hiyo zimeanguka na nyingine zipo hatarini kuanguka kwa sababu ya maji yaliyojaa ndani.”

“Baadhi ya watu wameokolewa na Jeshi la Zimamoto na kupelekwa mtaa wa pili wa Gama,” alisema Elizabeth.

Mwananchi mwingine, Adam Peter anayeishi mtaa wa Mhongolo alisema jana mchana maji yalianza kupungua lakini wana hofu kutokana na wingu lililopo kwamba mvua inaweza kuendelea na kusababisha madhara makubwa zaidi.

“Kwa kweli hali ni mbaya sana tunaiomba Serikali itusaidie angalau madaraja yaliyopo yajengwe upya kwani haya yalijengwa mwezi wa tatu hayajasaidia chochote kwani ni mafupi sana hayapeleki maji,” alisema Adam.

Share.

About Author

Leave A Reply