Friday, August 23

Uchumi wa Tanzania unaathiriwa na sera zisizotabirika- IMF

0


Shirika la Fedha Duniani (IMF) limesema kuwa uchumi wa Tanzania unaathiriwa zaidi na sera za uchumi zisizotabirika na serikali kuingilia katika soko.

Taarifa hiyo kwa mujibu ya tovuti ya Bloomberg ni kutokana na ripoti ya IMF ambayo Tanzania ilizuia kuchapishwa kwake.

Serikali ya Tanzania ilizuia shirika hilo kuchapisha taarifa ya hali ya uchumi na sera za ubadilishaji wa fedha za kigeni. Hata hivyo, Bloomberg walipojaribu kuwasiliana na Msemaji wa Serikali ya Tanzania, Dk. Hassan Abbas kwa ajili ya kuzungumzia suala hilo, simu yake haikupokelewa.

Uchumi wa Tanzania umekumbwa na matatizo na mabadiliko ya mara kwa mara ya sera chini ya utawala wa serikali ya awamu ya tano, jambo ambalo limekuwa likikosolewa kuwa linahatarisha ukuaji wa uchumi.

Moja ya mambo ambayo yalizua gumzo, ni kuafuatia kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia kutakiwa kulipa kodi ya dola za Marekani milioni 190 (zaidi ya TZS trilioni 400). Hata hivyo, Acacia ilisema makubaliano yoyote yatakayofikiwa kati ya serikali na Barick Gold ambayo ndiyo kampuni mama, watayajadili kwanza.

Itakuwa vigumu kwa Tanzania kulifikia soko la kimataifa, ikichangiwa na kuwa imekuwa na changamoto katika kupata fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo, kufuatia sera mbalimbali za uchumi zilizopitshwa na serikali, alisema Jibran Qureishi, mchumi kutoka Nairobi, akizungumzia hatua ya serikali ya Tanzania kuzuia kuchapisha ripoti hiyo.

Changamoto nyingine zinazoweza kuukumba uchumi wa Tanzania ambao ni wa pili kwa ukubwa Afrika Mashariki kwa mujibu wa IMF ni ukuaji taratibu wa maboresho ya usimamizi wa fedha, na pia kuwa na uwekezaji ambao hautakuwa na marejesho yenye tija.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, athari za kiuchumi zitakuwa ni kubwa kama hatua za makusudi hazitachukuliwa kukabiliana na hali hiyo.

Msemaji wa IMF, Lucie Mboto Fouda amesema kuwa wadau wa maendeleo hawawezi kuzungumzia ripoti hiyo ambayo haikutoka rasmi, badala yake imevuja.

Mbali na Tanzania, baadhi ya nchini nyingine ambazo ni nchi wanachama wa IMF, zimewahi kuzuia kuchapishwa kwa ripoti zao.

Share.

About Author

Leave A Reply