Sunday, August 18

Tanzania yaporomoka nafasi 25 viwango vya Uhuru wa Habari Duniani

0


Tanzania imeporomoka kwa nafasi 25 katika viwango vya Uhuru wa Habari Duniani hadi nafasi ya 118 kwa mwaka 2019 kutoka 93 mwaka 2018 kati ya nchi 180.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka (Reportes Without Borders), sekta ya habari nchini Tanzania imekumbana na changamoto mbalimbali kufuatia kupitishwa kwa sheria inayoonekana kuwa kandamizi na kanuni zake, kufungwa kwa vyombo vya habari, na kufukuzwa nchini kwa wanahabari.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo mambo mengine yaliyochangia Tanzania kuporomoka kwa kiwango hicho ni tukio la kuvamiwa kwa Clouds Media Group mwaka 2017, kufungiwa kwa baadhi ya vyombo vya habari.

Kwa upande mwingine pia kuporomoka huko kumechangiwa na waendeshaji wote wa tovuti na blogu za habari kutakiwa kujisajili na kulipa ada ili kuweza kutoa huduma hiyo, jambo ambalo limeelezwa kuwa linaminya uhuru wa habari.

Novemba 2018 serikali ya Tanzania iliwashikilia watumishi wawili wa Tume ya Kulinda Waandishi wa Habari (CPJ), Angela Quintal na Muthoki Mumo ambao walikuja nchini kwa ajili ya kufahamu changamoto mbalimbali zinazowakumba waandishi wa habari. Baada ya watumishi hao kuachiwa, waliondoka nchini.

Tukio jingine lililotikisa sekta ya habari ni kupotea katika mazingira ya kutatanisha kwa mwandishi wa kujitegemea, Azory Gwanda aliyekuwa akichunguza mauaji ya viongozi wa serikali za mitaa mkoani Pwani.

CPJ pamoja na mashirika mengine ya kimataifa yamekuwa yakiitaka serikali ya Tanzania kufanya uchunguzi ili kuweza kubaini alipo mwandishi huyo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, matukio haya ambayo yameathiri sekta ya habari Tanzania, ndio chanzo kikubwa cha kuporomoka kwa viwango vua uhuru wa habari.

Share.

About Author

Leave A Reply