Tuesday, August 20

Tahadhari: Mikoa ya Mtwara na Lindi kukumbwa na Kimbunga (Kenneth)

0


Mikoa ya Lindi na Mtwara ipo hatarini kukumbwa na Kimbunga Kenneth ambacho kinaendelea kujijenga katika Bahari ya Hindi, na kitatokea kusini mwa bahari hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) Kimbunga Kenneth kwa sasa kipo umbali wa takribani kilometa 700 mashariki mwa Mtwara. Mifumo ya hali ya hewa inaonesha kimbunga Kenneth kilichopo eneo la kaskazini magharibi mwa kisiwa cha Madagascar kinaambatana na mvua kubwa na upepo mkali katika eneo hilo.

Aidha, vipindi vya upepo mkali unaofikia na kuzidi kasi ya kilometa 80 kwa saa vinatarajiwa kujitokeza katika ukanda wa pwani ya kusini (Lindi na Mtwara). Kimbunga hicho kinaendelea kutawala mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini, hivyo kusababisha ongezeko la mvua zinazoambatana na ngurumo za radi pamoja na upepo mkali kadri kinavyokaribia maeneo ya ukanda wa pwani.

Kimbunga Kenneth kinatarajiwa kufika kwanza nchini Msumbiji ambapo kitakuwa umbali wa kilomita 200 hadi ulipo mpaka wa Tanzania. Baada ya kutua katika eneo hilo kitapungua nguvu (lakini bado kitakuwa na madhara), na kwenda kwa kasi ya kilomita 100 kwa saa.

Kimbunga hiki kitakapoingia nchi kavu kikiwa na nguvu inayotarajiwa kitakuwa na madhara makubwa kwa maisha ya watu na mali zao.

Madhara yanayotarajiwa ni pamoja na mtawanyiko mkubwa wa mafuriko, uharibifu wa mali na makazi, kuezuliwa mapaa kutokana na upepo mkali, uharibifu wa mazao mashambani, miundombinu kutokana na mafuriko na upepo mkali.

Madhara mengine ni kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari katika kipindi kifupi (storm surge), kuathirika kwa shughuli za usafirishaji kwa njia ya anga, kwenye maji na nchi kavu inaweza kuathirika hasa katika mkoa wa Mtwara na maeneo jirani (umbali wa kilometa 500).

Tarehe 26 kimbunga hicho kinatarajiwa kupungua kasi hadi kufikia kasi ya kilomita 80 kwa saa, lakini kitaingia ndani ya pwani ya Msumbiji kwa umbali wa kilomita 250.

Mamalaka ya Hali ya Hewa Tanzania imewataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa pamoja na kuchukua tahadhari.

Share.

About Author

Leave A Reply