Tuesday, August 20

Sudan Kusini yaingia mkataba wa mabilioni na kampuni binafsi, ili iboreshe uhusiano wake na Marekani

0


JUBA: Serikali ya Sudan Kusini imeingia mkataba wa miaka miwili na kampuni ya ushawishi kutoka Marekani, ili kulisaidia taifa hilo changa la Afrika kuimarisha uhusiano wake na Marekani katika nyanja za kisiasa na kiuchumi.

Mkataba huo baina ya pande hizo mbili una thamani ya TZS bilioni 8.5 ($3.7m) umesainiwa katika ya Sudan Kusini na Kampuni ya Gainful Solutions, kampuni ambayo inaongozwa na aliyekuwa Balozi wa Marekani nchini Kenya, Michael Ranneberger.

Mbali na kuimarisha uhusiano na Marekani, pamoja na majukumu mengine mkataba huo unaeleza kuwa kampuni hiyo itakuwa na jukumu la kuchelewesha na kuzuia uanzishwaji wa mahakama mseto (hybrid court).

Mahakama hiyo inayokusudia kuanzishwa ni sehemu ya maridhiano ya amani nchini Sudan Kusini, ambayo inatarajiwa kuwawajibisha wale wote waliohusika katika uhalifu wa kivita, katika mapigano yaliyopelekea vifo vya zaidi ya watu 400,000 nchini humo.

Mkataba huo umesainiwa ikiwa ni wiki chache kabla, maridhiano ya amani hayajaisha muda wake, ambapo pia kiongozi wa upinzani, Reik Machar atarejea nchini humo, Mei 12 ambapo atatwaa wadhifa wa Makamu wa Rais katika serikali ya mseto.

Wadadisi wa mambo wamesema kuwa maridhiano hayo ya amani yanaweza yasisainiwe tena, kwani tayari serikali imesema kwamba haina fedha (TZS bilioni 657) ya kutekeleza maridhiano hayo.

Upinzani nchini Sudan Kusini wamekosoa mkataba huo ambao serikali imeingia, na kusema kuwa unaonesha kutokujiamini kwa serikali, na kwa namna gani wanajitahidi kuepuka kuwajibishwa, na kuipinga haki, alisema Henry Odwar, Makamu Mwenyekiti wa Upinzani.

Mkataba huo umeibua maswali kuhusu nia ya serikali kuhakikisha waathirika wa mapigano hayo waliouawa, kutoweka, kubakwa, kuumizwa wanapatiwa haki.

Aidha serikali imesema kuwa haina kusudio la kuzuia kabisa kuanzishwa kwa mahakama hiyo, badala yake ni lazima vipaumbele viangaliwe, na kwamba sasa wanaangazia zaidi usuluhishi kuliko kuadhibiana.

Mahakama hiyo ilitarajiwa kuwa imeanzishwa na kuanza kufanya kazi ndani ya mwaka mmoja baada ya maridhiano ya amani mwaka 2015, lakini Serikali ya Sudan Kusini ilichelewesha usainiwaji wa nyaraka muhimu (Memorandum of Understand), na upitishwa wa sheria ambayo ingepelekea kuanzishwa kwa mahakama hiyo.

Share.

About Author

Leave A Reply