Friday, August 23

Spika Ndugai na Waziri Lugola wasema ripoti ya CAG ina uongo

0


Katika vikao vya mkutano wa Bunge wa Bajeti ya mwaka 2019/20 vinavyoendelea sasa jijini Dodoma, jana suala la ripoti ya CAG liliibuka tena bungeni, ambapo ilielezwa kuwa, ripoti hiyo imesheheni uongo.

Waliotoa tuhuma hizo kuwa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ina uongo ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola na Spika wa Bunge Job Ndugai.

Kwa nyakati tofauti, wawili hao walisema kuwa ripoti hiyo ina masuala ambayo si ya kweli.

Kwa upande wa Waziri Lugola, yeye alimkosoa CAG, ambapo alisema kwamba hajawahi kuona mtu muongo nchini Tanzania kama CAG, kwani amewasilisha kwa Rais ripoti yenye uongo kuwa jeshi la polisi limelipa fedha kununua sare ambazo ni hewa.

Katika ripoti yake, Prof. Mussa Assad (CAG) alisema kuwa Jeshi la Polisi lililipa Sh. bilioni 16 kwa ajili ya ununuzi wa sare za polisi bila kuwapo kwa ushahidi wa ununuzi.

Lakini waziri mwenye dhamana jana alikanusha madai hayo na kusema kuwa hakuna sare hewa, na kwamba yupo tayari kuandamana na CAG, au maofisa wake kwenye kwenye maghala ya polisi ili akaone sare hizo.

Sijawahi kuona mtu muongo kama CAG kwenye nchi ya Tanzania. Haiwezekani sare zinazodaiwa kuwa hewa, mimi nimekwenda kwenye makontena na ma-godown ya Polisi nimekuta sare nyingi ambazo zimeletwa, halafu CAG anapelekea taarifa kwa Mhe. Rais, ya uongo, kwamba hakuna sare za jeshi la polisi.

Aliendelea kusema kwamba yupo tayari kuweka uwaziri wake rehani, ikiwa itabainika kuwa taarifa zake za ukaguzi kuhusu sare hewa za jeshi la polisi zilizogharimu Sh16bilioni ni ya kweli.

Alisema kama anasema uongo, atajivua nguo aambatane na maofisa wa CAG kwenye stoo kuu wakaangalia makontena zaidi ya 15 yenye futi 40 na maghala 5 ambayo yamesheheni sare za jeshi hilo.

Licha ya kuwa CAG alieleza udhaifu mwingine katika ripoti yake kuhusu Jeshi la Polisi, waziri huyo hakuzungumzia masuala hayo mengine, ikiwa ni pamoja na vifaa vya utambuzi wa alama za vidole vyenye thamani ya Sh1.73 bilioni havikufungwa kwenye magereza 35 kama ilivyoainishwa badala yake, vilihifadhiwa katika ofisi ya upelelezi Makuu ya Polisi.

Mambo mengine yaliyoibuliwa na CAG ni malipo ya Sh604.39 milioni kwa ajili ya mafunzo kwa wataalamu 30 hayakufanyika.

Alisema jeshi la Polisi lilishindwa kuionyesha timu yake ya ukaguzi zilipo monita 58 za kompyuta aina ya Dell zenye thamani ya Sh159.16 milioni zilizopelekwa kwenye kitengo cha cha uchunguzi wa kisayansi cha Makao Makuu ya Polisi (Forensic).

Pia, alisema monita 213 za kompyuta aina Dell zilizolipiwa Sh195.22 milioni kwa mzabuni Lugumi Enterprises Limited lakini mzabuni hakuzikabidhi.

Kwa upande wake Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema wapo watu wanaowaaminisha Watanzania kuwa kila kinachoandikwa kwenye ripoti ya CAG, ni ukweli asilimia mia, jambo ambalo si sahihi.

Spika Ndugai alikuwa anamkosoa Mbunge Zitto Kabwe ambaye alisema kuwa amekuwa mwepesi wa kuuputisha umma kwa kutumia ripoti zinazotolewa na ofisi ya CAG.

Kiongozi huyo wa Bunge alisema kwamba kinachotolewa na CAG ni hoja, ndio sababu kamati zenye dhamana, Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Bunge Hesabu za serikali za Mitaa (LAAC) hukaa na kuichambua ripoti hiyo.

Watu wanawaaminisha Watanzania kuwa kila kilichoandikwa na CAG au ofisi yake ni ukweli asilimia 100. Sio hivyo, yapo mambo mle si kweli hata kidogo. Zile ni hoja, ndio maana kamati za PAC na LAAC zinachambua kila kitu, alisema Ndugai.

Share.

About Author

Leave A Reply