Thursday, August 22

Si sahihi Mawaziri kujibu ripoti ya CAG

0


Mwaka 2018, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka alisema kuwa sio sahihi kwa mawaziri kumjibu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwani kuna taratibu za kushughulikia ripoti hiyo mara tu ikishafika bungeni.

Kaboyoka akizungumza na waandishi wa habari mwaka jana alisema kuwa mawaziri waliokwisha kufanya hivyo au waliopanga kufanya hivyo wamekiuka taratibu, na kwamba ni muhimu taratibu zikafuatwa, sio kila mtu aibuke na kumjibu CAG, kwani kwa kufanya hivyo nchi haitatawalika.

Kiongozi huyo alitoa maelezo hayo kufuatia hatua za baadhi ya mawaziri kuwa waliibuka na kujibu hoja zilizoibuliwa na CAG kwatika ripoti iliyoishia mwaka 2016.

Licha ya kuwa jambo hilo lilitolewa ufafanuzi katika kipindi hicho, baada mawaziri wameendelea kujibu hoja za CAG, ambapo hivi karibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola alisimama bungeni na kusema kuwa CAG ni muongo, kwani hoja ya sare hewa za polisi alizozisema sio kweli, kwani sare hizo zipo.

Mwenyekiti wa PAC alisema, kutokana na kwamba ripoti ya CAG ina taratibu zake juu ya namna ya kushughulikiwa, ikiwa ni kamati kukaa pamoja na CAG na maafisa Masuuli ili kupitia hoja hizo, hivyo jambo lolote litakalosemwa na waziri nje ya utaratibu, yatakuwa ni mawazo yake yeye.

Ripoti ya CAG ina taratibu zake, tukifanya kazi nje ya taratibu, hii nchi haitatawalika. Na CAG ni jicho la Bunge, sio adui wa serikali, kwani yeye huiambia serikali kuwa huku kuna mambo hayaendi vizuri, hela za umma hazitumiki vizuri. Hivyo inaifanya serikali irudi nyuma ikaangalie, alisema kiongozi huyo.

Aliongeza kuwa, kama wizara itaona kuwa imefanya kitu fulani, lakini sivyo ripoti ya CAG inavyoonesha, taarifa itapelekwa kwenye kamati za PAC na LAAC, ambapo baada ya kuwasilisha nyaraka, CAG atakwenda kujiridhisha kama kweli jambo hilo limefanyia kweli.

CAG ndiye pekee mwenye uwezo wa kupangua hoja za kwenye ripoti na si mtu mwingine yeyote, alisema Kaboyoka.

Share.

About Author

Leave A Reply