Sunday, August 18

Sevilla FC ya Hispania itaweza kuivunja rekodi ya Simba Uwanja wa Taifa?

0


DAR ES SALAAM, Tanzania -Kampuni ya SportPesa kwa kushirikiana na Ligi Bora duniani ya LaLiga tunaileta nchini klabu ya Sevilla FC.

Ziara hiyo inayokwenda kwa jina la ‘LaLiga World SportPesa Challenge” itawashuhudia mabingwa hao mara tano wa UEFA Europa League wakiumana na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, Simba SC, siku ya Alhamisi ya Mei 23 katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.

Ikiwa na mastaa wake wa kikosi cha kwanza kama vile Jesus Navas, Wissam Ben Yedder, Andre Silva, Pablo Sarabia na wengine wengi, Sevilla itatembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini, kufanya semina elekezi kwa viongozi wa soka nchini pamoja na kliniki za soka kwa wachezaji na makocha.

Taarifa ya ujio huo ilitolewa rasmi Aprili 17 Bungeni jijini Dodoma ikihudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Hamis Kigwangala, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mh. Juliana Shonza pamoja na Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa SportPesa Ndugu, Tarimba Abbas.

Rekodi ya Kimataifa

Simba wameithibitishia Tanzania na Afrika kwa ujumla kuwa moja ya timu ngumu kufungika kwenye uwanja wake wa nyumbani katika michezo  ya kimataifa iliyocheza msimu huu.

Wekundu hao wa Msimbazi wametoa dozi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Mbabane Swallows (Swaziland), Nkana FC (Zambia), JS Soura (Algeria), Al Ahly (Misri ) bila kusahau ule ushindi maarufu dhidi ya AS Vita kutoka Jamhuri ya Congo uliowapa tiketi ya kufuzu hatua ya robo fainali huku wakienda sare ya 0-0 na TP Mazembe kwenye hatua ya robo fainali.

Tanzania itafaidika vipi?

Ziara hii ya kimichezo nchini inatarajiwa kuitangaza Tanzania kimataifa kama moja ya sehemu bora kwa timu kubwa za Ulaya kutembelea baada ya msimu au kabla kuanza kwa msimu mpya.

Si tu hivyo, bali wadau wa soka nchini kama vile viongozi wa TFF na Vilabu, makocha na wachezaji watapata nafasi ya kujifunza mbinu za kisasa za uendeshaji soka nje na ndani ya uwanja.

Ujio wa Sevilla pia unatarajiwa kuwa fursa pekee kuvitangaza vivutio vyetu vya Utalii nchini bila kusahau utamaduni wetu uliotukuka.

Sevilla itakuwa timu ya kwanza kutoka LaLiga na timu ya pili kutoka barani Ulaya kutembelea Tanzania kwa udhamini wa SportPesa baada ya Everton kufanya hivyo Julai 2017 ambapo wapenzi wa soka nchini walipata nafasi ya kumshuhudia Wayne Rooney akiichezea Everton mechi yake ya kwanza baada ya miaka 13 kupita.

Je, Sevilla itakuwa timu ya kwanza ya kimataifa kuifunga Simba kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam msimu huu?

Share.

About Author

Leave A Reply