Thursday, August 22

Serikali yataja muda wa kuwasili nchini ndege nyingine mbili mpya

0


Ndege nyingine mpya aina ya Bombardier D8 Q400 na Boeing B787-8 Dreamliner zinatarajiwa kuletwa mwishoni mwa mwaka huu.

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye amesema hayo bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Khadija Nassir Ali (CCM).

Mbunge huyo alihoji kwa kuwa serikali inaendelea na ununuzi wa ndege; haioni ni wakati muafaka kuhakikisha ndege hizo zinakwenda kila mkoa wenye kiwanja na nchi jirani kusaidia kushusha gharama za usafiri.

Nditiye alisema matarajio ya serikali ni kuwa ujio wa ndege hizo utawezesha Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kuwa na ndege za kutosha na kutoa huduma za usafiri wa anga kwa ufanisi na tija.

Alisema ATCL itakuwa na mtandao wa safari mikoa mingine na safari kikanda na kimataifa.

“Uwapo wa ndege mpya za kutosha utaiwezesha ATCL kuhimili ushindani wa kibiashara katika utoaji huduma za usafiri wa anga katika masoko ya ndani, kikanda na kimataifa,” alisema.

Alisema upanuzi mtandao wa huduma za usafiri wa anga katika kila mkoa wenye kiwanja cha ndege na nchi jirani, unatekelezwa kwa mpango mkakati wa ATCL wa miaka mitano unaoishia mwaka wa fedha 2021/2022 pamoja na mpango wa biashara unaoandaliwa kila mwaka.

Alisema hadi sasa ATCL inasafirisha abiria katika mikoa tisa na nchi tano. Mikoa hiyo ni Dodoma, Mwanza, Kagera, Kigoma, Mbeya, Kilimanjaro, Zanzibar, Tabora na Mtwara.

ATCL inatoa huduma Hahaya (Moroco), Harare (Zimbabwe), Bujumbura (Burundi), Entebbe (Uganda) na Lusaka nchini Zambia. Utoaji wa huduma unazingatia uwapo abiria wa kutosha kuifanya kampuni hiyo ijiendeshe kwa ufanisi.

Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Bulembo (CCM) alitaka kufahamu kwa nini bei ya tiketi za ndege ATCL isishuke kuwezesha watu wengi kumudu usafiri.

Naibu waziri alisema bei hupungua kutokana na soko.

Alisema ATCL iko kwenye ushindani na mashirika mengine yakitoa huduma, bei itashuka. Ndege hizo mbili zikiwasili zitafanya nchi kuwa na ndege nane zilizonunuliwa na serikali ya awamu ya tano.

Ndege zilizopo sasa ni Airbus A220-300 iliyopokewa Januari mwaka huu. Nyingine ni Bombardier Dash 8 Q400 tatu zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja, Boeing 787-8 Dreamliner moja yenye uwezo wa kubeba abiria 262 na Airbus A220-300 yenye uwezo wa kubeba abiria 132 kila moja.

Chanzo: HabariLeo

Share.

About Author

Leave A Reply