Sunday, August 25

Serikali yaeleza madhara ya uvaaji wa miwani za urembo

0


Serikali imewatahadharisha wananchi juu ya uvaaji wa miwani za urembo, kwamba wanajiweka katika hatari kubwa ya kupata matatizo ya macho.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ambapo alieleza kuwa, utumiaji wa miwani hizo na matumizi ya dawa za macho kiholela vimekuwa ni vibabishi vikubwa vya ongezeko la watu wenye matatizo ya macho nchini.

Waziri Ummy alisema hayo wakati akizindua kambi ya kutibu macho iliyoandaliwa na Asasi ya Maendeleo ya Wanawake Mkoa wa Tanga (TAWODE), kwa kushirikiana na Taasisi ya Bilal Muslim Mission ya Tanzania chini ya udhamini wa shirika la Better Charity kutoka Uingereza.

Katika zoezi hilo, Waziri Ummy alisema kuwa kati ya watu 100 waliojitokeza, wanne kati yao walikuwa na tatizo la macho, na kwamba idadi hiyo inaweza ikaongezeka kama wananchi hawatachukua hatua, zikiwamo za kutokuvaa miwani kiholela na matumizi ya dawa za macho ambazo hazijatolewa na wataalamu.

Watu wanashauriwa kuvaa miwani za jua, lakini baada ya kuonana na wataalamu ambao hutoa ushauri wa miwani bora ya kuvaa, kwa kuzingatia kiwango cha giza au mwanga kwenye macho.

Aliongeza kuwa mambo mengine yanayochangia kuharibika kwa macho ni watu kula vyakula visivyo na vitamini A na kula kwa uchache mboga za majani na matunda.

Aidha aliwataka wananchi kuwa na tabia ya kupima afya za macho yao, kwani wale ambao wanawahi hospitali matatizo yao yanaweza kupona kabisa.

Katika kambi hiyo ya siku nne, watu 2,000 watapimwa macho na kupatiwa matibabu bure, ikiwa ni pamoja na kupatiwa miwani ya kusomea, kuona na ya jua.

Share.

About Author

Leave A Reply