Sunday, August 18

Sababu ya ATCL kuhamishiwa Ofisi ya Rais kutoka Wizara ya Ujenzi

0


Serikali imeeleza sababu ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kuhamishwa kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwenda katika Ofisi ya Rais.

Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika aliliambia Bunge kuwa ni uamuzi wa Rais katika kuamua ni shughuli gani wizara inatakiwa kutekeleza na ipi haitakiwi.

Wizara zote zinapokea maelekezo kutoka kwa Rais, na wala hii sio mara ya kwanza jambo kama hili linatokea. Kwa mujibu wa sheria, ni Rais pekee mwenye mamlaka ya kugawa majukumu kadiri atakavyoona inapendeza, alisema Waziri Mkuchika.

Waziri huyo alilazimika kutoa ufafanuzi huo bungeni wakati wa Bajeti ya Ofisi ya Rais ambapo pia alitolea mfano wa Kituo cha Uwekezaji cha Tanzania (TIC) ambacho karibuni kilihamishiwa katika ofisi ya Waziri Mkuu kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara.

Aidha aliongeza kuwa, changamoto mbalimbali zilizokuwa zikilikumba shirika hilo zinaweza kuwa ndio sababu ya Rais kuamua kuliweka chini ya ofisi yake.

Awali Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo) alidai kuwa serikali ilihamishia shirika hilo katika Ofisi ya Rais ili Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) asiweza kukagua matumizi ya shirika hilo.

Kwa mujibu wa Zitto shirika hilo lilihamishwa kwa notisi ya Gazeti la Serikali No. 252 la 2018, ili fedha zilizotumika kununua ndege mpya na matumizi mengine ya shirika hilo yasiweze kukaguliwa.

Hadi sasa serikali imeshakabidhiwa ndege sita kati ya ndege nane ilizopanga kununua ambapo Zitto amesema kuwa TZS trilioni 1 ilitumika katika manunuzi hayo, lakini hazijakaguliwa na CAG.

Mwaka huu serikali imeliomba Bunge kuidhinisha TZS bilioni 500 kwa ajili ya kununua ndege nyingine, lakini inashangaza kuwa wameliweka shirika hilo chini ya Ofisi ya Rais ambapo hakuna mtu anayeweza kuhoji matumizi yake. Mnaficha nini? alihoji Zitto Kabwe.

Katika uchambuzi wa ripoti ya CAG ya mwaka 2017/18, Mbunge Zitto Kabwe alimsihi CAG kufanya ukaguzi maalum katika shirika hilo ili wananchi wa waweze kujua matumizi ya fedha za kodi zao.

Ripoti ya CAG iliyotolewa mapema juma lililopita imeeleza kuwa ATCL ni moja kati ya mashirika 14 ya umma yenye matatizo ya kifedha na hasara hadi kusababisha madeni zaidi ya mitaji yao.

Kwa sasa shirika hilo linalofufuka baada ya kutofanya vizuri sokoni kwa miaka mingine lina ndege nane ambazo ni, Bombardiers Q-400s tatu, Airbus (A200-300) mbili, Fokker50, Fokker28 na Boeing 787-8 Dreamliner.

Share.

About Author

Leave A Reply