Sunday, August 25

Njia 5 za kumshawishi mwajiri akuongezee mshahara

0


Kuongezewa mshahara ni jambo ambalo kila mfanyakazi analifurahia, lakini sio kila mfanyakazi anajua ni namna gani ya kuzungumza na mwajiri wake ili mshahara wake uongezwe.

Katika mchakato wa kuomba kuongezewa msharaha, kuna mambo ya msingi ya kuzingatia ili kufanikiwa. Lakini jambo la msingi zaidi, unapokwenda ofisini kwa mwajiri wako na ombi hilo, usiende na jibu ukiwa tayari umeliandaa, kwamba lazima akubali.

Ukiwa na matarajio makubwa sana, unaweza kuichukia kazi yako, au kumchukia mwajiri wako pale ambapo atakupa jibu tofauti na ulilokuwa nalo kichwa.

Utendaji kazi : Unapokwenda kuomba kuongezewa mshahara, ni muhimu kumuonesha mwajiri wako ni kwa kiasi gani umeweza kufikia malengo yaliyokuwa yamewekwa (KPIs).

Orodhesha chini mambo yato ambayo umeyafanya na kuisaidia kampuni kukua, hasa kwa kuongeza mapato. Pengine mwajiri wako anafahamu kuwa umefanya mambo kadhaa makubwa na unastahili nyongeza ya mshahara, lakini anaweza asikupe au akachelewesha hadi wewe mwenyewe udai.

Hali ya Kampuni: Kweli, unaweza ukawa umefanya mambo makubwa sana, na kustahili nyongeza ya mshahara, lakini kama kampuni kwa wakati huo haiko vizuri kifedha, huwezi kupata nyongeza hiyo.

Unashauriwa kutokuomba nyongeza ya mshahara wakati kampuni inapunguza wafanyakazi, unapata hasara, au ipo katika wakati mgumu unaofanya mambo yasiende sawa.

Subiri hadi wakati mambo yanakwenda vizuri, mapato yanaongezeka, huu ndio wakati mwajiri wako anaweza kukaa mkazungumza na mkaelewana.

Ijue Thamani Yako: Kabla ya kwenda kuomba nyongeza ya mshahara, hakikisha umefanya uchunguzi ili uweze kujua watu waliopo kwenye sekta moja na wewe, au kwenye nafasi kama yako, wanalipwa shilingi ngapi.

Kama mwajiri wako anakulipa kiwango kidogo tofauti na mshahara halisi ama wa fani yako, kiwango chako cha elimu au nafasi iliyopo, itakuwa rahisi kwako kudai nyongeza ya mshahara.

Jadili: Wakati mwingine mwajiri wako anaweza kuwa tayari kukupa nyongeza, lakini sio yote kama uanavyotaka. Endapo hili likitokea, jiandae kufanya majadiliano nae ili mfikie makubaliano ambayo wote mtaridhika.

Wakati mwingine mwajiri anaweza akakuongezea posho za malazi, usafiri, chakula na kadhalika. Yote haya yanategemeana na ninyi mtakavyo afikiana.

Ongeza Elimu: Wakati mwingine mwajiri wako hakuongezei mshahara kwa sababu ya kiwango chako cha elimu.

Kwa kuongeza kiwango chako cha elimu au ujuzi katika eneo lako la kazi, unakuwa umejiweka katika mazingira mazuri zaidi ya kudai nyongeza ya mshahara na ukakubaliwa.

Baadhi ya waajiri mbali na kuridhia kukuongezea mshahara unapohitimu, pia hujitolea kugharamia masomo yako endapo utaomba.

Unapoomba kuongezewa mshahara, unashauriwa kutokutumia vitisho, mfano kutishia kuacha kazi endapo ombi lako halitakubaliwa. Hii ni hatari kwani inaweza kupelekea kupoteza kazi, na hata mshahara huo uliokuwa unauona ni mdogo.

Kuna msemo wa kiswahili unasema Mwenge hauruki Kijiji, hivyo na wewe unapotaka kuomba nyongeza ya msharaha hakikisha unakwenda hatua kwa hatua. Usiruke ofisi ya mkuu wa idara yake, na kwenda kwa mkurugenzi mkuu, au kwa bosi aliye juu ya mkuu wa idara yako.

Kwa kuanza na kiongozi aliyekaribu nawe inaweza kukusaidia ombi lako kufanikiwa.

Share.

About Author

Leave A Reply