Saturday, August 17

Hatua chache za kufuata unapopoteza kitambulisho cha taifa

0


Karibuni serikali imetangaza kuanza kwa zoezi la usajili wa kadi za simu (laini) kwa kutumia alama za vidole, ambapo ili kufanikisha zoezi hilo, kila anayemiliki kadi ya simu atatakiwa kuwa na kitambulisho cha taifa au namba ya kitambulishi, au Kitambulisho cha mpiga kura.

Watu wengi wamekuwa wakilalamika kwamba ama hawana vitambulisho vya taifa kwa sababu tangu wamesajiliwa hawakuwahi kuletewa vitambulisho hivyo.

Lakini wengine wameeleza kwamba vitambulisho vyao vimepotea na hivyo kutaka kufahamu hatua wanazotakiwa ili kuweza kupata vitambulisho vipya.

Mwombaji aliyepoteza kitambulisho chake kwa kuibiwa au kwa majanga, atapaswa kufika katika ofisi ya NIDA kwenye wilaya anayoishi na kuthibitisha taarifa zake kabla ya kupewa barua ya utambulisho kwa Polisi, barua ambayo itakuwa na namba yake ya utambulisho.

Kupitia barua hiyo Polisi watampatia uthibitisho wa upotevu wa kitambulisho chake “Police Loss Report”. Kisha mtuamiaji atapaswa kufanya yafuatayo ili kupata kitambulisho kipya:

1. Mtumiaji atawasilisha ripoti ya upotevu kutoka Polisi; katika ofisi ya NIDA wilaya anayoishi na kujaza fomu maalumu.

2. Atatakiwa kulipia benki ada ya TZS 20,000/- kama gharama za kuchapisha upya kitambulisho chake.

3. Akisha kufanya malipo, atawasilisha stakabadhi ya malipo ya benki na kupata stakabadhi ya serikali kutoka ofisi ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

4. Baada ya kukamilika utaratibu huo, atapewa muda wa kusubiri kabla ya kufika kwenye ofisi ya NIDA kupewa kitambulisho kingine.

Muhimu kufahamu; Vitambulisho vya Taifa kwa mara ya kwanza hutolewa bure kwa raia, na pindi kinapochapishwa upya raia hana budi kulipia kufidia gharama za uchapaji. 

Kwa mwenye kitambulisho ambaye ambaye anataka kubadili taarifa zake na hivyo kuhitaji kitambulisho kuchapishwa upya atafanya yafuatayo:-

1.Mwombaji atapaswa kuandika barua NIDA kueleza sababu za msingi za kubadilisha taarifa zake katika mfumo na kuambatanisha hati msingi za kisheria zenye kuruhusu kufanya hivyo. Mfano iwapo atataka kubadili majina lazima kufika na hati ya kisheria ijulikanayo kama “deed poll”.

2.Mwombaji atajaza fomu ya maombi katika ofisi ya NIDA kwenye Wilaya anayoishi

3. Atatakiwa kulipia benki ada ya shs. 20,000/- kama gharama za kuchapisha upya kitambulisho chake.

4. Akisha kufanya malipo, atawasilisha stakabadhi ya malipo ya benki na kupata stakabadhi ya serikali kutoka ofisi ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

5. Baada ya kukamilika utaratibu huo, atapewa muda wa kusubiri kabla ya kufika kwenye ofisi ya NIDA kupewa kitambulisho kingine.

Share.

About Author

Leave A Reply