Sunday, August 25

ONGEZEKO LA WATU, WATUMIAJI WA SIMU KUKUZA BIASHARA ZA MTANDAONI AFRIKA

0


Na Jumia Tanzania


Kuendelea kukua kwa ongezeko la idadi ya watu na watumiaji wa simu za mkononi barani Afrika kuna mchango kwenye ukuaji wa biashara kwa njia ya mtandao. Hilo linaenda sambamba na ueneaji wa huduma za mtandao wa intaneti ambao umebadili namna waafrika wanavyotumia simu zao za mkononi hivi sasa. 

Hivi karibuni Jumia, mtandao unaojihusisha na uuzaji na manunuzi ya bidhaa mtandaoni, ulizindua ripoti kuhusu sekta ya bidhaa za simu kwa mara ya kwanza nchini Tanzania. Ripoti hiyo imeangazia masuala mbalimbali kwenye setka hii pamoja na mchango wake katika shughuli za kijamii na kiuchumi nchini. Ripoti hiyo pia imeangazia namna watanzania wanavyotumia simu na teknolojia ilizoambatana nazo kama vile huduma za fedha na biashara za mtandaoni. 

Akizungumzia juu ya ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Jumia Tanzania, Zadok Prescott amebainisha kuwa uwasilishwaji huo umekuja katika kipindi ambacho wanaendesha kampeni ya ‘Wiki ya Simu’ itakayohusisha uuzaji wa simu kwenye mtandao wao kwa kushirikiana na makampuni tofauti ya simu nchini.

“Jumia inaamini kwamba soko la simu ni miongoni mwa sekta kubwa kwenye nchi zinazoendelea barani Afrika, na ina mchango mkubwa kwenye kuziwezesha sekta zingine. Wiki ya Simu itafanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania kuanzia Machi 24 mpaka 30, kampeni ambayo ni kubwa kabisa ndani ya mwaka ikiwa imejikita kwenye bidhaa moja pekee. ‘Jumia Mobile Week’ itawawezesha watanzania kujipatia mapunguzo na ofa mbalimbali kwenye bidhaa za kutoka kampuni tofauti za simu,” alisema Prescott.

Sekta ya bidhaa za simu Afrika ina thamani ya bilioni $110 

Hivi sasa, idadi ya watu barani Afrika imefikia bilioni 1.27 ambapo takribani watu bilioni 1.04 wanatumia simu za mkononi, sawa na ueneaji kwa asilimia 82. Kuongezeka kwa idadi ya watu na mtandao wa intaneti kwenye maeneo mbalimbali kumeendelea kuifanya sekta hiyo kuwa na tija zaidi. Sekta hii ina mchango mkubwa kwenye maisha ya kila siku ya watu kama vile huduma za fedha kwa njia ya simu. Ambapo nchini Tanzania pekee, zaidi ya watu milioni 40 waliripotiwa kuunganishwa na huduma za simu za mkononi wakati kiasi cha zaidi ya shilingi trilioni 50 zikitumwa kwa njia ya simu. 

Mwaka 2016, huduma za teknolojia ya simu zilizalisha kiasi cha dola za Kimarekani bilioni 110 katika uchumi wa nchi za Kiafrika zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara, sawa na asilimia 7.7 ya pato la ndani la taifa. Mchango wa sekta ya simu kwenye pato la taifa unatarajiwa kukua na kufikia dola za Kimarekani bilioni 142, sawa na asilimia 8.6 ya pato la ndani la taifa, kufikia mwaka 2020, kwani nchi nyingi zitakuwa zikinufaika na maendeleo katika uzalishaji na ufanisi utakaoletwa na kuongezeka kwa matumizi ya simu za mkononi. 


Ueneaji wa watumiaji wa simu Tanzania unakaribiana na wa Afrika

Hivi karibuni, Tanzania ilitangaza kuongezeka kwa idadi ya watumiaji wa simu na kufikia zaidi ya milioni 40, ambayo ni sawa na ueneaji kwa asilimia 72, asilimia 10 pungufu ya ueneaji wa bara zima la Afrika ambao umefikia asilimia 82. 


Uwepo wa ushindani wa bei na motisha kwa wateja kwenye soko la simu umekuwa na mchango mkubwa katika unafuu wa upatikanaji wa bidhaa hizo. Kitu kingine cha muhimu, ni uwepo wa huduma mpya zinazotambulishwa na kampuni tofauti za mitandao ya simu zimekuwa ni kichocheo kikubwa kwa watanzania wengi kumiliki simu za mkononi.

Simu kutoka bara la Asia zatawala kwenye mtandao wa Jumia

Bidhaa za simu kutoka bara la Asia zinaongoza kwa kuwa miongoni mwa simu zinazonunuliwa zaidi kwenye mtandao wa Jumia. Kampuni zinazofanya vizuri ni pamoja na Tecno, Samsung, Lenovo, na Infinix, ukilinganisha na simu kutoka nchi za Magharibi (Ulaya na Marekani). Infinix ni simu inayoongoza kwa mauzo katika nchi 10 ambazo Jumia inaendesha shughuli zake, wakati Tecno ikiwa ni kinara katika mtandao huo nchini Tanzania.  

Simu kutoka bara hilo zimefanikiwa kulitawala soko la Afrika kwa sababu zimeweza kuendana na mahitaji yake. Nchi nyingi za Kiafrika bado zinaendelea, ni dhahiri kwamba nguvu ya manunuzi bado ni ndogo. Kikubwa zaidi, simu zao ni za gharama nafuu na zinapatikana kwa urahisi, karibuni kila mji ukilinganisha na simu kama vile iPhone ambazo hupatikana kwenye miji mikubwa na ya kibiashara pekee. 


Zaidi ya watu bilioni 4 duniani wanatumia intaneti

Idadi ya watumiaji wa mtandao wa intaneti duniani imevuka bilioni 4, idadi ambayo ni sawa na zaidi ya nusu ya watu wote duniani. 


Tanzania nayo inakua kwa kasi kwa upande wa idadi ya watumiaji wa simu na mtandao wa intaneti katika ukanda wa Mashariki na Afrika kwa ujumla. Mapema mwaka huu, TCRA iliripoti juu ya kuongezeka kwa idadi ya watumiaji na ueneaji wa intaneti kufikia milioni 23 sawa na asilimia 45 mwaka 2017, kutoka watumiaji milioni 7.5 sawa na asilimia 17 mwaka 2012. 


Simu ni mkombozi kwa watanzania kiuchumi na kijamii

Idadi ya watumiaji wa simu za mkononi inatarajiwa kuvuka bilioni 5 kufikia mwaka 2019. 

Nchini Tanzania, idadi kubwa ya watumiaji wa simu za mkononi wameonekana kukitumia kifaa hiki kwa manufaa mbalimbali ya kijamii na kiuchumi. Ukiachana na kuzungumza, kutumiana jumbe za maandishi au kuingia kwenye mitandao ya kijamii, baadhi ya watanzania wameanza kufanya shughuli zao za manunuzi mtandaoni, tena kwa kutumia simu zao za mkononi. 


Mwaka 2017, asilimia 83 ya wateja wa Jumia walifanya manunuzi kwa kutumia simu za mkononi. Hii ni ishara kwamba idadi ya watanzania inazidi kuongezeka katika kutumia simu za mkononi kurahasisha shughuli zao za kila siku. 

“Biashara kwa njia ya mtandao bado ni sekta mpya Tanzania, ambayo ipo kwenye hatua za awali za ukuaji. Naamini kwamba ueneaji wa huduma ya mtandao wa intaneti utachochea ukuaji wa sekta hii. Barani Afrika hivi sasa, ni idadi ndogo sana ya manunuzi yanafanyika mtandaoni, yaani kununua bidhaa kwa kutumia intaneti,” alielezea na kuhitimisha, “kuna ukuaji mkubwa wa idadi ya watu wanaomiliki simu za mkononi, hususani simu janja. Hii ni hatua muhimu kwenye sekta. Lakini bado idadi ya wamilikaji wa simu janja ni ndogo, changamoto ambayo Jumia tumeiona na tungependa kuitatua kwa kuhakikisha kwamba zinapatikana kwa gharama nafuu na urahisi. Na hilo ndilo dhumuni la kampeni ya ‘Wiki ya Simu’.’”Read More

Share.

About Author

Comments are closed.