Sunday, August 25

UNESCO yaonya athari za mapinduzi ya kidigitali katika uhifadhi wa nyaraka

0


Tume ya Taifa ya UNESCO Tanzania imeonya uwepo wa athari zitokanazo na mapinduzi ya matumizi ya mfumo wa kidjitali katika kuhifadhi nyaraka muhimu za serikali na sekta binafsi.

Tahadhari hiyo imetolewa na Lusajo Mwaitekele wakati akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mawasiliano na Habari kutoka Tume ya Taifa ya UNESCO Tanzania- NATCOM, Christina Musaroche, katika semina kuhusu masuala ya uhifadhi wa taarifa kwa kutumia mfumo wa kidijitali iliyoandaliwa na tume hiyo.

“Urithi wa kidijitali unaohifadhiwa kwa ajili ya manufaa ya vizazi vijavyo uko hatarini kupotea kutokana na kasi ya mabadiliko ya mfumo huo yanayotokea mara kwa mara yasiyoepukika,” amesema.

Akizungumza katika semina hiyo, Mhifadhi wa Makumbusho ya Taifa Dkt. Amandus Kweka amesema athari hizo zinatokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya utengenezaji wa vifaa vya kielektroniki vinavyotumika kuhifadhi nyaraka hizo ikiwemo simu na kompyuta. 

“Serikali inahamasisha jamii ihamie kwenye mfumo wa dijitali bila ya kuwa na mikakati ya kuhifadhi taarifa za nyuma. Inatakiwa tuwe na maandalizi ya namna gani tunatunza taarifa muhimu ili ziweze leta faida kwa vizazi vya baadae,” amesema na kuongeza.

“Serikali na wadau mbalimbali wanatakiwa kuwa na mikakati itakayoendana na kasi ya mabadiliko ya mfumo huo hasa katika kuhifadhi taarifa muhimu katika vyombo vya kidijitali ikiwemo simu na kompyuta.”

Naye Mhifadhi kutoka Makumbusho ya Taifa, Flower Manase ameishauri jamii hasa serikali na taasisi binafsi kubadili namna ya kuhifadhi taarifa zao kila mara ili kukwepa usumbufu ikiwemo kupotea kwa taarifa zao za muhimu.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.