Thursday, August 22

Serikali yatakiwa kuondoa changamoto wanazokutana nazo watoto wa kike

0


Shirika lisilo la kiserikali inaloshughulika na masuala ya vijana Femina Hip limeitaka serikali na jamii kuondoa changamoto wanazokabiliana nazo watoto wa kike wakiwa katika kipindi cha hedhi, ikiwemo kuhakikisha wanapata taulo za kujihifidhi, vyoo wanavyotumia kuwa salama na maji ya uhakika ili waepukane na magonjwa hatarishi. 

Wito huo umetolewa leo na Mwenyekiti wa Femina Hip, Sauda Simba wakati akizungumza katika hafla ya utoaji tuzo kwa washindi wa shindano la uandishi wa Insha kuhusu hedhi lililoshirikisha wanafunzi wa shule za sekonfdari kutoka mikoa 15 nchini, iliyofanyika jijini Dar es Salaam. 

Simba amesema bado watoto wa kike wanakabiliwa na changamoto wakiwa katika siku zao, ikiwemo kukosa pedi, maji safi na salama kitendo kinachohatarisha usalama wa afya zao. 

“Kwenye nchi zinazoendelea hedhi salama ni tatizo, takwimu zinaonyesha mtoto wa kike mmoja kati ya 10 hawahudhurii shule wakiwa katika siku zao kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kukosa pedi, maji safi na salama wakiwa shuleni na umbali wa shule,” amesema na kuongeza. 

“Tunaweza kupaza sauti zetu ili jamii na serikali isikie shida zetu na kutatua shida za watoto wa kike. Wazazi walezi na jamii ijue ni jukumu lao na si kuiachia serikali peke yake.”

Aidha, amewataka wazazi na walezi kuwa wazi kwa watoto wao wa kike kuhusu masuala ya hedhi salama ili kuwaondolea usumbufu wanapofikwa na hali hiyo, kwa kuwa shindano hilo limebainisha kuwa wasichana wengi hufikwa na hali hiyo pasipo kujitambua au kuwa na uelewa wa suala hilo. 

Kiongozi wa Timu ya Nguvu ya Binti kutoka Femina Hip, Lydia Charles amesema shindano hilo lililenga kuleta uelewa pamoja na kubaini changamoto kuhusu masuala ya hedhi wanazokabiliana nazo watoto wa kike katika jamii.

Kwa upande wake, Balozi wa masuala ya hedhi salama, Badru Juma ameitaka serikali na jamii kutatua changamoto wanazokutana nazo watoto wa kike hasa wa kijijini.  

Na Regina MkondeRead More

Share.

About Author

Comments are closed.