Thursday, August 22

CAG aagizwa kukagua miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Tabora

0


Kamati ya Bunge Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalumu wa miradi yote ya maendeleo katika Manispaa ya Tabora ili kujiridhisha kama fedha zilizotumika katika utekelezaji wake unalingana na thamani ya mradi.

Maagizo hayo yametolewa jana na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Abdallah Chikota kwa wajumbe wengine mara baada ya kutembelea miradi kwa ajili ya kukagua utekelezaji wake ambao katika miradi mitatu ya Manispaa hiyo waliyotembea waliikuta katika hali isiyoridhisha.

Alisema katika mradi wa kwanza wa bwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji cha mpunga la Inala ambapo ujenzi wake umegharimu milioni mia sita(600,000,000/-) lakini kwa miaka zaidi ya mitano halijaanza uzalishaji.

Chikota alisema kitendo cha kusababisha kuchelewa kuanza kwa sababu ya kushindwa kulipa fidia kwa baadhi ya wakulima ili mradi huo uanze kazi kinarudisha nyuma maendeleo  ni sawa na kuchezea fedha za umma.

Katika mradi wa pili ambao ni ujenzi wa Hospitali ya Manispaa ya Tabora ambapo jengo la OPD ambalo ujenzi umeishia kujenga msingi na kusimamisha nguzo.

Alisema kuchelewa kwa mardi kunawakosesha huduma za afya wananchi na hivyo kuwapelekea kwenda mbali kutafuta matibabu.

Mradi mwingine ambao LAAC ilibaini mapungufu ni ule wa maduka 29 ambao hakuna vyoo kwa ajili ya wateja.

Chikota alisema inawezekani mradi wa Halmashauri unaanzisha bila hata kuwa na huduma ya vyoo, huku mtu binafisi harusiwi kuanzisha biashara bila choo.

Alisema Kamati imebaini kuwa hakuna mipango vizuri ya kuanzisha miradi mbalimbali ndio maana mingi haikamiliki kwa wakati na hivyo kusababisha wananchi kuendelea kukosa huduma ambazo zilikusidia kupelekwa kwao.

Kamati hiyo pia imeiagiza Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi) kuhakikisha kuwa hadi kufikia Mwezi Juni mwaka huu inapangua watumishi waliomo katika mendeo ya  Uhasibu , Mipango , uchumi na Biashara baada ya kushindwa kusimamia vizuri miradi ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi) Joseph Kakunda aliihakikishia Kamati hiyo kusimamia utekelezaji wa maagizo iliyotoa kwa ajili ya kuboresha utendaji ambao utasaidia kuharakisha maendeleo kwa wananchi.

Na Tiganya Vincent, TaboraRead More

Share.

About Author

Comments are closed.