Sunday, August 25

Road 2 Russia: Ballon D Or ya Neymar ipo Russia

0


Kama kuna wachezaji wapo kwenye presha kubwa basi hatuwezi kuacha kumtaja Neymar Jr. Makelele mengi na sala za wabrazil huenda zikamwendea Neymar.

Roberto Carlos yeye anasema hakuna haja ya kumtegemea zaidi Neymar. Yeye anaona Brazil inajiweza. Anasema Brazil ni kikundi cha watu na sio timu ya mchezaji mmoja.

Kauli ya Carlos haijalandana sana na Pele. Pele ameweka jukumu la kombe la dunia kwenye miguu ya Neymar. Amesema anakumbuka vyema 2002 Ronaldo alipeleka kikombe nyumbani baada ya kumnyanyasa Oliver khan. Na ametamka wazi wazi kuwa huu ni mwaka wa Neymar

Wakati Pele na Carlos wakikinzana kauli kauli nyingine tata ni Ya Ronaldo De lima. De lima alipoulizwa kuhusu usajili wa gharama kwa Neymar alijibu kwa kuzunguka sana. Alijibu akasema “maamuzi ya usajili ya mchezaji ni bahati nasibu, hata mimi niliwahi kuhama kutoka Barcelona kwenda Inter lakini kipindi ligi ya Italia ikiwa na Ushindani”

Mantiki ya hii kauli ni nini? Kwamba kuhama sio tija ila unakwenda wapi. Ni kama hakupendezwa na uhamisho wa Neymar kwani alikimbia ushindani. Aliniamini kuwa Neymar alipaswa kwenda ligi yenye ushindani. Ni kweli ilikuwa uamuzi mgumu kwa Neymar kugomewa marashi ya waarabu wa PSG.

Brazil inamtegemea Neymar. Hili lipo wazi kila mwaka lazima awepo mfalme wa taifa. Neymar ana kikosi bora sana msimu huu ambacho kinaweza kumsaidia yeye kutwaa kombe la Dunia pia kupata nafasi kubwa ya kutwaa Ballon D Or. De lima mwenyewe alitwaa tuzo ya Dunia.

Walimshauri wengi kuwa aondoke nje ya kivuli cha Messi ili aweze kutwaa Mafanikio Binafsi. Ameondoka sawa lakini binafsi naona njia nyepesi ya yeye kupata ubingwa ambayo atawatambia sana messi na ronaldo. Messi ni kama amekwisha kata tamaa na timu yake ya taifa. Neymar bahati yake ipo Russia.

Muunganiko mzuri wa mabeki wa katikati.
David Luiz amecheza na Thiago Silva kwa kipindi fulani, Thiago Silva na Marquinhos wamecheza muda mrefu sana klabuni PSG hivyo wanafahamiana vyema.

Mabeki wa pembeni bora kabisa duniani. Unapotaja beki namba 3 bora duniani utakuwa umetenda dhambi kubwa ya kufungiwa kushabikia mpira usipomtaja Marcelo. Faida ngingine ni beki wa pembeni Dani Alves ambaye ana uzoefu mkubwa wa michuano yote duniani akiwa tayari amekwisha pitia ligi kubwa 3 barani ulaya.

Viungo bora
Muunganiko mzuri wa Casamero na Fernandinho ni pilipili tosha kwenye dimba la kati. Ni viungo bora kwa sasa. Wana uzoefu wa michezo migumu. Pia kuna wachezaji wanaofanya vyema kwenye vilabu vyao kama Wilian (Chelsea), Roberto Bobby Firmino (Liverpool), Paulinho (Barcelona). Bila kudharau nafasi ya Douglas Costa.

Pia kuna vipaji vya kutosha. Huwezi kuacha kumtaja Philippe Coutinho kati ya wachezaji waliobarikiwa kipaji haswa. Gabriel Jesus amekuwa na uchu sana wa kupata mafanikio. Licha ya kuwa na umri mdogo lakini kujituma kwake pamoja na kipaji alicho nacho vitaleta hamasa kubwa sana katika safari yao ya Russia.

Mwaka 2002 wakati Brazil inabeba ubingwa haikuwa na wachezaji Mastaa wengi sana. Wachezaji 12 tu ndio waliokuwa wametoka nje ya Brazil, Dida alikuwa Brazil, Kaka nae alikuwa Sao Paolo, Gilberto Silva nae alikuwa Brazil. Wengine walikuwa vilabu vya kawaida tu, Dinho alikuwa PSG kama Neymar tu kwa sasa, Juninho alikuwa Middlesbrough, Cafu alikuwa Roma, De lima Alikuwa Inter, Carlos alikuwa Madrid.

Neymar afanyeje?

Neymar ni moja kati ya wachezaji tishio duniani. Ni fundi. Anajua mpira na ana uwezo binafsi. Kila mtu anajua Neymar ni fundi. Nadhani hana haja ya kuonyesha kuwa anajua kupiga chenga na kanzu. Aachane na hayo mambo sio muda wake. Hayo mambo afanye akiwa anacheza na Nantes huko. Sasa ni muda wa kumuonesha Messi na Ronaldo kuwa alichelewa kuja kwenye uso wa soka lakini yeye ni mbrazil. Na jadi ya wabrazil ni kombe la dunia na Joga Bonito.

Kwa kikosi chao hiki, na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja naamini wanaweza kufika mbali sana hata kutwaa ubingwa wanaweza pia kama wakicheza kitimu. Waache kuiga waliowatangulia. Kumekuwa na kasumba kuwa usipocheza kama Ronaldo au Kaka basi huna heshima Brazil. Mimi naamini heshima ya Brazil ni Ubingwa tu na sio kingine.

Kocha afanyeje?
Arudishe Samba tu.

Imeandaliwa na Priva Abiud
Instagram PrivaldinhoRead More

Share.

About Author

Comments are closed.