Thursday, August 22

Mchawi wa taifa stars ni nani?

0


Kinachonichekesha ni kwa namna tunavyotwanga kokoto kwenye kinu. Kila siku tunalaumu mtwangio wetu haufanyi kazi bila kujua sisi ndo chanzo. watanzania tunataka kuvuna shamba tusilolipanda. Wanaorudisha soka letu nyuma ni wale wale wanaotaka lisonge mbele. Leo hii mtu anaidhihaki taifa stars ni wazi kwamba jukumu la taifa stars ni la watu 30 waliotwa kucheza soka. Yaani sisi tumejitenga na taifa stars. Tunachoamini kwa kuwa tumeleta kisu basi jioni tunatarajiwa kula nyama. Mtu huyo huyo anayeidhihaki Taifa Stars ndiyo yule yule aliyeenda taifa kuwashabikia waarabu. Uzwazwa wa namna gani huu?

Wengine Tunajifanya tunaumizwa sana na soka letu ikiwa hata viwanjani hatuendi.

Shida nyingine ni Viongozi. Tutajenga vipi soka ikiwa tunajenga matumbo yetu? Abdi Banda aliniambia kinachotuponza Watanzania ni kukosa imani. Viongozi wengi kanjanja, mashabiki sio wavumilivu na hawajitoi, wachezaji wengi pia hawajitambui. Ngoja niwambieni kitu wabongo wenzangu.

Kuna vilabu vina matokeo mabovu kuliko Stars. Jenga picha mshabiki wa Derby County ambaye alipanda na timu yake ligi kuu na ikashikilia mkia mpaka iliposhushwa? Chukulia mfano mshabiki wa Westbrowm? Au jenga picha mshabiki wa Wolfsburg ambaye alibeba ubingwa 2009, 2014 akamaliza wa pili, kisha mwaka jana kaponea chupuchupu kushuka daraja kwa kufanikiwa kushinda hatua ya mtoano. Wolfsburg mwaka huu wapo kwenye hatari ya kushuka daraja. Lakini mashabiki hawakati tamaa wanakesha na timu zao hadi zinashuka daraja na wanakwenda nazo daraja la kwanza huko.

Iweje sisi ambao tunajua wazi kuwa ligi yenye imejaa ukata na miundo mbinu mibovu lakini tumekaa kukosoa kana kwamba sisi ni wamarekani?

Sakata la matokeo mabovu kwa stars halijaanza jana. Sio geni kwetu.

Ukweli ni kwamba Tatizo kubwa la soka letu ni Simba na Yanga. Nawaambie ukweli siku Simba au Yanga mmoja wao akapotea kwenye Ramani yetu ya soka basi mafanikio yatakuja. Hatuwezi kufanikiwa tukiwa na timu zinazovutana mashati kwa ushabiki wa kizwazwa.

Nikwambie ukweli soka lina faida kubwa sana kwa taifa. Kule England kila wikiendi watu zaidi laki 2 wanakwenda viwanjani. Hawa wote wanalipa zaidi ya laki za kitanzania. Kodi zinakatwa. Wachezaji wanapokea hela kila siku kodi zinakatwa. Juzi niliongea na Abdi Banda akaniambia nyuma yake kuna watu zaidi ya 50 wanaomtegemea. Kimahesabu ukiwa na ligi yenye timu 20 kimsingi hapo umetoa ajira kwa Vijana 2000. Hao vijana 2000 kila mmoja nyuma yake kuna watu watatu mpaka watano amewaajiri (wakala, Meneja, daktari, mshauri wake wa kisheria,) hapo hapo hao niliowataja wana watu zaidi ya 5 wanaowategemea, huyu mchezaji nae ana watu sio chini ya 10 wanamtegemea. Hujapunguza ufukara kwa vijana wenye vipaji?

Lakini huu mnyororo ninaousemea hauwezi kukua tu kirahisi. Ni lazima kuwe na uwekezaji wa maana na kuachana na fikra mbovu mbovu za usimba na uyanga.

Kule ulaya wale mashabiki unao waona uwanjani sio kwamba hawana Tv nyumbani kwao. Ila wameshazoea ndio maisha yao. Sisi leo hii ukienda uwanjani unakuta watu 2000. Ni Kichekesho. Ule uwanja tumejenga wa kazi gani sasa? Wenzetu wanabeba watoto wao wanaenda nao uwanjani. Hivi wewe mwanaume wa dar ukaenda na mtoto wako ukamlipia 2000 baba akalipa 5000 unapungukiwa nini? Hiyo 7000 ungeenda kuinywea bia au hata kuhonga.

Huyu mtoto unayekwenda nae uwanjani akiwa na miaka 10 akifikisha miaka 20 hawezi kuangalia mpira kwenye Tv. Hauwezi kumvutia.

Tumejenga misingi gani? Misingi yetu tumempa mchawi mtoto atusaidie kumlea.

Leo hii mechi inachezwa taifa kuna mtu amekaa hapo kizuiani anaangalia kwenye Tv.. kweli? Nani aliyewadanganya Simba na Yanga kukubali kuonesha mpira unaochezwa ndani ya Dar kurushwa ndani ya Dar? Nani atakwenda uwanjani? Kufanya nini? Pesa za kuendesha soka tunategemea vijisenti mtakavyopokea kwa hao wanaorusha haya matangazo? Nani kakwambia? Mechi ya Dar Es Salaam inapaswa itazamwe kwenye Tv kwa mtu aliyepo Mwanza au Mbeya huko na sio hapa hapa. Mpira ni mashabiki na si vingenevyo. Mikataba ya matangazo ya televishen ambayo haina mipaka ni sawa na fisi aliyeshikwa kwenye mtego kwa sababu ya makombo. Acheni tamaa.

Wenzetu ulaya wapo hivi.

Wanamzoesha mtoto kwenda uwanjani. Hawana muda na Tv. Wenzetu ulaya wanarusha soka kwenye TV ili kujitangaza nje ya mipaka yao. Ili wawafikie wale waliopo mbali. Je sisi tunamtangazia nan? Nani nje anaangalia huu uroaroa wetu?

.

Kuna haja ya kufanya jambo kujua namna ya kukuza soka letu. Lakini kuna uozo uliopo kwenye vilabu vikubwa. Ndio maana nasema hata ulaya vilabu vikubwa viliporomoka akina Blackburn, St Etienne, akina Deportivo la Coruna, Malmo FF zilishuka daraja, Akina Newcastle n.k

Tunahitaji watawala wapya ili kujenga tabaka jipya la Mashabiki.

Hatuwezi kujenga taifa Stars inayotokana na simba na yanga. Kuna mtu ameniambia eti Banda na Msuva na Samata walitusaidia? Nikamwambia ukiwa na meno 10 mabovu na mawili mazuri bado hutoweza kula nyama vizuri.

Kesho nitaendelea
Priva ABIUD 0763370020Read More

Share.

About Author

Comments are closed.