Wednesday, August 21

RC WANGABO AZIGEUKIA NGOs NA CSOs KUHAMASISHA UANZISHWAJI WA VIWANDA KUPAMBANA NA UMASIKINI

0


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amezitaka asasi za kiraia na mashirika yasiyo ya kiserikali kuchukulia juhudi za uanziswaji wa viwanda nchini unaofanywa na serikali kama suala mtambuka na ukombozi kwa mwananchi katika kupambana vita dhidi ya Umasikini huku wakizingatia utunzaji wa mazingira na kushirikiana na SIDO.


Amesema kuwa takwimu zinaonesha kwamba takribani hekta 300,000 hadi 400,000 za misitu nchini huharibiwa kwa kuchoma Mkaa. Hivyo njia nyingine na muhimu kuokoa mazingira yetu ni kwa kuanzisha viwanda vya kutengeneza Mkaa kwa kutumia marando ya Mbao, Pumba za Mpunga, Mabua ya mahindi n.k. malighafi ambazo hupatikana kwa wingi Mkoani kwetu.

“Kwa sababu hiyo ninapenda kutoa wito kwa NGOs na CSOs kushiriki kwenye kampeni hii ya uanzishwaji wa viwanda yenye kaulimbiu ya Mkoa wetu, Viwanda vyetu kwa kuanzisha viwanda. Viwanda tunavyovilenga ni vile vidogo vya thamani ya kuanzia milioni 2 hadi Milioni 10,” Alisisitiza.


Kwa upande wake Meneja wa SIDO Emanuel Magere amesema kuwa asasi pamoja na mashirika hayo yamekuwa yakitoa elimu mbalimbali kutegemea matatizo ama changamoto za wananchi lakini imefika wakati kutambua kuwa, wananchi hao wanahitaji pia elimu ya ujasiliamali ili kuanzisha viwanda, na kuziomba taasisi za fedha kuweza kutoa mikopo kwa wanaohitaji kuanzisha viwanda.


“Mwamko katika uazishwaji wa viwanda sio mkubwa sana, wengi wamekuwa wakijiwekeza kwenye sekta ya huduma mfano, mashule, migahawa, maduka na huduma mbalimbali ambayo “return” yake inakuwa ya haraka kuliko viwanda na pia changamoto ya masoko ya bidhaa za ndani ya mkoa kutoka kwa bidhaa za nje ya mkoa ama nje ya nchi imekuwa ni changamoto kwa mkoa,” Alimalizia.


Katika kuhimiza ushirikiano Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda amezitaka NGO na CSO hizo kuweza kufika kwenye ofisi za kiserikali ili kuweza kujitambulisha shughuli wanazofanya na kujitokeza kwenye songambele mbalimbali zinazofanywa na halmashauri katika ujenzi wa madarasa ya shule na vituo vya afya ili michango yao ijulikane na sio kusubiri kutafutwa na serikali.


Katika utekelezaji wa viwanda 100, ndani ya kipindi cha miezi minne kuanzia Disemba mwaka 2017 hadi 26, Machi, 2018 Mkoa wa Rukwa umezalisha viwanda vidogo 51 huku lengo la Mkoa ni kuwa na viwanda vingi zaidi ili kuchangia kwa kiasi kikubwa lengo la Kitaifa la kufikia nchi ya Uchumi wa Kati wa Viwanda ifikapo 2025.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.