Thursday, August 22

Aliyekuwa Kamishna Madini kusomewa maelezo ya awali Aprili 2

0


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Aprili 2, 2018 kumsomea maelezo ya awali (PH), aliyekuwa Kaimu Kamishna wa Madini kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Ally Samaje.
Mwendesha Mashtaka kutoka Takukuru, Leonard Swai ameyasema hayo leo Machi 28, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mwambapa, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kusomewa mshtakiwa maelezo yake.
Kwa mara ya kwanza, Samaje alifikishwa mahakamani hapo, Februari 9 mwaka huu kujibu mashtaka mawili ya matumizi mabaya ya madaraka yanayomkabili.
Swai alidai mahakamani hapo kuwa kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa na Hakimu Mfawidhi, Victoria Nongwa ila kwa sasa imehamishiwa kwa Hakimu Mwambapa.
“Kesi hii ilikuwa mbele ya Hakimu Mfawidhi, Victoria Nongwa, ila kwa sasa imehamishiwa kwako, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali, ” amedai Swai.
Baada ya Swai kutoa maelezo hayo, Hakimu Mwambapa aliahirisha kesi hiyo hadi April 2, mwaka huu, ambapo upande wa mashtaka utamsomea maelezo hayo.
Katika kesi ya msingi, Swai alidai kuwa mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo kati Aprili 9 na Juni 21, 2013 Makao Makuu ya Wizara ya Nishati na Madini iliyopo wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.

Chanzo: MwananchiRead More

Share.

About Author

Comments are closed.