Tuesday, August 20

WANAKIJIJI CHIKONGO WASHUPALIA MAPATO NA MATUMIZI

0


Kamati ndogo ya kuchunguza mapato na matumizi imeundwa katika mkutano
wa hadhara wa kijiji cha Chikongo baada ya Wananchi kuchachamaaa kwa
kuikataa taarifa ya Serikali ya kijiji.

Sakata hilo limeibuka kwenye mkutano wa robo ya tatu ya mwaka katika
Kijiji cha Chikongo kilichopo kata ya Mkoreha mbele ya Afisa Tarafa ya
Mihambwe Gavana Emmanuel Shilatu baada ya Wananchi kutokuwa na imani
na ripoti iliyosomwa kutowaridhisha .

Kutokana na tafran hiyo Afisa Tarafa ya Mihambwe Emmanuel Shilatu
aliagiza mara moja iundwe kamati ndogo itakayopitia mapato na
matumizi ya Kijiji hicho jambo ambalo liliungwa mkono na Wananchi.

Gavana huyo alitaka kamati hiyo ihusishe viongozi wa kata, Serikali
ya Kijiji, baadhi ya Wananchi na wajumbe wa kamati ya ujenzi ili
kumaliza utata huo na ukweli ujulikane

“Yapo madai ya mkutano mkuu wa kijiji hauitishwi kwa mujibu wa
kalenda, Wananchi hawasomewi mapato na matumizi, Madai hayo ni
ukiukaji wa sheria. Napendekeza iundwe kamati hapa hapa. Ipekue
hesabu kisha ije na majibu ya kuridhisha” Alisema Gavana Shilatu.

Katika hatua nyingine Gavana Shilatu kupitia mkutano huo aliwataka
Wakulima kuendelea na kazi zao za kilimo na wajasiliamali kuendelea
kupatiwa vitambulisho vya shughuli zao.

“Mkulima ahakikishe analima, Mjasiriamali apatiwe kitambulisho.
Tunahitaji kila Mwananchi awe mlinzi wa amani. Wote tukifanya kazi
ndipo tutakapoinua uchumi wa nchi.” alieleza Gavana Shilatu.

Katika mkutano huo wa Kijiji ulihudhuliwa na Afisa Tarafa Mihambwe,
Diwani kata ya Mkoreha, Mtendaji kata na Wajumbe wa Serikali ya Kijiji
cha Chikongo.

Share.

About Author

Leave A Reply