Wednesday, August 21

Uhamiaji watakiwa kuwa makini suala zima la ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi

0


Maafisa waandamizi na watendaji wa Idara ya Uhamiaji wametakiwa kuwa
makini katika suala zima la ulinzi pamoja na usalama wa mipaka ya nchi
ili kuliepusha Taifa kuvamiwa na wageni wasiokuwa waaminifu.

Kufanya hivyo kutalisaidia Taifa pamoja na wakazi wake kuendelea
kuishi katika mazingira salama muda wote na kufanya kazi zao bila ya
hofu.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd.Shaaban
Seif Mohamed alieleza hayo wakati akizungumza na maafisa na watendaji
wa idara ya Uhamiaji katika ukumbi wa Ofisi hizo zilizopo Kilamani
Mjini Zanzibar.

Alisema Idara ya Uhamiaji ni taasisi muhimu na nyeti katika
kuhakikisha mipaka ya nchi inakuwa salama hivyo kuna haja ya kufanya
Doria au ukaguzi kwa uwaangalifu katika mipaka ya Nchi kavu na
baharini ili kuweka udhibiti wa wahamiaji haramu,na kufanya uvamizi.

“Nitoe mfano kuna changamoto ya bandari bubu zinazopokea wageni bila
ya kuwepo maafisa kutoka idara ya Uhamiaji jambo ambalo ni hatari na
linafaa kuachwa mara moja”. Alisema Katibu Mkuu Shaaban.

Nd. Shaaban alifahamisha kwamba suala la ulinzi wa mipaka katika
ndani ya nchi linahitaji ushirikiano wa pamoja kati ya idara hiyo na
wananchi wake sambamba na watendaji kutoka Serikali Kuu.

Akijibu baadhi ya Changamoto zinazoikabili idara hiyo Katibu Mkuu
alisema viongozi wanaosimamia majukumu mbali mbali wanapaswa kuzisemea
Changamoto hizo kwa viongozi wanaohusika ili ziweze kupatiwa ufumbuzi
na aliwahidi maafisa hao kwa yale yanayoweza kupatiwa ufumbuzi
Serikali itayachukulia hatua.

Akisoma taarifa ya Idara ya Uhamiaji Naibu Kamishna utawala na Fedha
Ali Suleiman Nassor alimuelezea Katibu Mkuu Shaaban kuwa idara ya
uhamiaji Zanzibar imefanikisha kuwakamata wageni 205 na kuchukuliwa
hatuwa za kisheria ambapo kati yao 26 waliondoshwa nchini na 109
walilipia vibali,15 walishtakiwa Mahakamani ,21 waliachiwa Huru baada
ya uchunguzi na wageni 34 bado uchunguzi unaendelea .

Naibu Kamishna Ali alieleza idara ua Uhamiaji katika Kuimarisha Ulinzi
na Usalama imewatambua na kuwaoredhesha wahamiaji walowezi 1, 281,
Unguja na Pemba kati ya hao 668 wameshasajiliwa .

Vile vile alieleza katika suala zima la utoaji wa vibali , Idara
imetoa jumla ya vibali 1,116 kwa wageni kwa shughuli mbali mbali
ikijumuisha vibali 143 vya daraja A, 536 vya daraja B, 437 vya daraja
C, 225 hati za ufuasi na 250 hati za msamaha.

Alisema katika mwaka wa Fedha 2018/2019 Idara ilipangiwa kukusanya
Shillingi 30,001,727,413/- kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Machi 2019
ambapo hadi sasa imekusanya Jumla ya Shillingi 26,104,134, 382.42/-
sawa na asilimia 87% ya malengo ya Makusanyo yote.

Akigusia Changamoto zinazoikabili Idara hiyo Naibu Kamishna alizitaja
Changamoto hizo ikiwemo Ufinyu wa Afisi ya Uhamiaji Mkoa wa Mjini
Magharibi ,kukwama kwa utaratibu wa kumalizia upatikanaji wa eneo la
Kitogani kwa ajili ya Ujenzi wa eneo la Chuo cha Uhamiaji pamoja na
ukosefu wa boti kwa ajili ya kufanyia doria.

Wakichangia katika Kikao hicho Maafisa wamemtaka Katibu Mkuu Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuzitembelea Afisi nyengine za
Wilaya Unguja na Pemba ili kujionea hali halisi ya Mazingira ya Kazi .

 Naibu Kamishna utawala na Fedha Ali Suleiman Nassor Kushoto akimpokea Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Ndugu Shaaban Seif Mohamed aliyefika Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji Zanzibar kuzungumza na Makamanda na Watendaji wa Jeshi hilo.

 Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Ndugu Shaaban Seif Mohamed akitia saini kitabu cha Wageni alipofika Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji Zanzibar kuzungumza na Makamanda.

 Naibu Kamishna utawala na Fedha wa Uhamiaji Zanzibar Ali Suleiman Nassor akitoa Taarifa ya uwajibikaji wa Jeshi hilo kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Ndugu Shaaban Seif Mohamed alipofika kuzungumza nao.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Ndugu Shaaban Seif akizungumza na Makamanda na Watendaji wa Jeshi la Uhamiaji Makao Makuu yao Kilimani Mjini Zanzibar. Picha na – OMPR – ZNZ.

Share.

About Author

Leave A Reply