Monday, June 17

MKURUGENZI TEMEKE AWATAKA WANANCHI KUJIHADHARI NA MLIPUKO WA KIPINDIPINDU

0


Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Lusubilo Mwakabibi  awatahadharisha wakazi wote wa Manispaa na viunga vyake kuchukua tahadhari ya mlipuko wa  ugonjwa wa Kipindupindu .

Alibainisha kuwa kukithiri kwa uchafu katika maeneo mengi ni sababu mojawapo inayopelekea mlipuko wa magonjwa ikiambatana na matumizi ya maji yasiyo safi na salama iwapo yatatumiwa katika chakula au mtu kunywa bila ya kuchemshwa kwa kiwango kinachohitajika,alibainisha kwamba usafi wa mazingira ni wa msingi zaidi ili kujilinda na magonjwa ya mlipuko.

“Manispaa ya Temeke imejipanga kwa kutoa elimu ya uhamasishaji  na tayari wadau wa Afya wameanza kutembelea nyumba kwa nyumba katika maeneo yote yaliyoathirika sambamba na  ugawaji wa dawa za usafi ili kuangamiza mazalia”.Alibainisha zaidi

Tangu ugonjwa wa kipindupindu uliporipotiwa kwa Manispa ya Temeke tarehe 20/04/2019 wagonjwa 48 wamehisiwa mpaka sasa, na kati yao vipimo 10 vimeonesha uwepo wa ugonjwa huo na vifo vilivyoripotiwa ni 2 tu.

Nae Mratibu wa ufuatiliaji magonjwa wa Manispaa ya Temeke Prisca Uswege alibainisha kuwa mpaka sasa nyumba 400 zimetembelewa  na wakazi 123 wamepatiwa  elimu ya namna ya kujikinga na mlipuko huo sambamba  na ugawaji wa water guard pamoja na dawa ya Chlorine.

Nae Mganga Mkuu wa Manispaa ya Temeke Dr.Gwamaka Mwabulambo alisema “tayari kuna kambi maalumu iliyopo katika Hospitali ya Temeke kwaajili ya magonjwa ya mlipuko ambapo  matibabu na uangalizi kwa wagonjwa hao hufanyika kwa urahisi zaidi”.

Dr. Mwabulambo alibainisha zaidi kwamba dalili za ugonjwa wa kipindupindu ni pamoja na kuharisha mfululizo, kutapika,macho kudidimia ndani, kinyesi na matapishi yenye rangi kama ya maji ya mchele, pamoja na ngozi kusinyaa.

Pamoja na hayo ameeleza  namna ya kujikinga na mlipuko huo kwa kunawa mikono kwa maji safi na salama kwa sabuni kabla ya kuandaa chakula ama kumlisha mtoto,kunawa mikono kwa maji safi na salama baada ya kutoka chooni au kumsafisha mtoto aliyejisaidia,kusafisha matunda  ama vyakula vibichi kama matunda na mbogamboga, kuhakikisha unatumia choo kwa usahihi,kula chakula cha moto,kufunika chakula kilichoandaliwa tayari kwa  kula,na ukiona mtu anatiririsha au kutapisha choo,toa taarifa haraka kwenye ofisi za serikali ya mtaa au kata zilizokaribu na nawe.

Kipindupindu kitakwisha iwapo mazingira bora ya kukiepuka yatakuwepo huku jamii nzima ikipewa elimu ya namna ya kujilinda na magonjwa ya mlipuko sambamba na kuhaikisha kanuni za Afya zinazingatiwa.

Share.

About Author

Leave A Reply