Sunday, August 18

Jeshi la Wokovu kufadhili vijana 300 kupata mafunzo ya Ufundi Stadi

0


Kaimu Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Dar es Salaam Florence Kapinga akizungumza katika hafla ya makubaliano ya VETA kusomesha vijana 300 wenye mahitaji maalum katika mafunzo ya ufundi stadi katika eneo la Hoteli na Utalii , mafunzo hayo yamefadhiliwa na jeshi la Waokovu hafla hiyo imefanyika katika kumbi wa jeshi hilo, jijini Dar es Salaam.

Na Chalila Kibuda, Globu ya Jamii

Jumla ya vijana 300 wanaotoka katika mazingira magumu wilaya ya Temeke wanatarajia kupata ufadhili wa kusoma mafunzo ya ufundi stadi katika eneo la hoteli na utalii kupitia Jeshi la Wokovu. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa program ya kuwezesha vijana hao jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Dar es Salaam Florence Kapinga alisema kuwa mradi huo wa miaka minne unaotarajiwa kuanza mwezi Mei, mwaka huu unalenga kuongeza fursa za ajira na kipato kwa vijana wenye mahitaji maalum wilayani Temeke.

Amesema VETA itashirikiana na Jeshi la Wokovu na Manispaa ya Temeke ambapo VETA itatoa mafunzo huku manispaa ya Temeke ikifanya uchambuzi wa wahitaji kutoka katika manispaa hiyo. Kapinga alisema kuwa mradi huo umekuja kwa wakati mwafaka ambapo mamlaka inafanya jitihada kuhakikisha elimu na mafunzo ya ufundi stadi inafikia makundi yote katika jamii na kuiunga mkono sera ya Serikali ya kuhakikisha Tanzania inafikia uchumi wakati.

Amesema VETA itahakikisha mafunzo hayo yanatolewa kwa ubora na kuwezesha vijana hao kupata ujuzi unaoendana na mahitaji ya sasa yasekta ya hoteli na utalii iliwaweze kuajirika. Kanali Mkuu wa Jeshi la Wokovu Tanzania, Wayne Bungay amesema jeshi hilo limekuwa likitoa mchango wake katika elimu hasa katika kuwawezesha watoto na vijana na kwamba anaamini mradi huo utaleta matokeo chanya kwavijana watakaonufaika pamoja na familia zao.

Bungay amesema vijana hao wakihitimu wana uhakika wa ajira kutokana na mawasiliano ya hoteli mbalimbali ambazo zimekubali pindi wanapohitimu watafanya mafunzo ya vitendo pamoja na kupata ajira. Amesema mradi huo umetoa kipaumbele kwa wasichana na kwamba asilimia 60 ya wanufaika itakuwa wasichana, na asilimia asilimia 40 wavulana na asilimia 5 kati yao ni wenye ulemavu.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Mhandisi Damas Primy alitoa shukrani kwa Jeshi la Wokovu kwa ufadhili huo na kwamba utasaidia kupunguza idadi ya vijana wasiona ujuzi wala ajira wilayani kwake. Alisema wilaya itahakikisha zoezi la utambuzi wa vijana hao unafanyika kikamilifu kwa kuhusisha viongozi wa mitaa ili ufadhili huo uwafikie wahitaji.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Mhandisi Damas Primy akizungumza katika hafla ya makubaliano ya kati VETA na Jeshi kusomesha vijana 300 wenye mahitaji maalum kwa vijana wa manispaa ya Temeke, jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Dar es Salaam Florence Kapinga na Kanali Mkuu wa Jeshi la Wokovu Tanzania, Wayne Bungay wakisaini makubaliano ya jeshi hilo kusomesha vijana 300 katika katika mafunzo ya ufundi stadi katika chuo VETA cha Chang’ombe , jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Dar es Salaam Florence Kapinga akipeana mkono wa shukurani na Katibu Mkuu wa Jeshi la Waokovu Col. Samwel Makami mara baada ya kusaini makubaliano ya kunufaika mafunzo kwa vijana wa wenye mahitaji maalumu katika Manispaa ya Temeke.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Mhandisi Damas Primy na Kanali Mkuu wa Jeshi la Wokovu Tanzania, Wayne Bungay wakisaini makubaliano ya jeshi hilo kusomesha vijana 300 katika katika mafunzo ya ufundi stadi katika chuo VETA cha Chang’ombe , jijini Dar es Salaam.
Watendaji wa VETA na Jeshi la Waokovu pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Mhandisi Damas Primy wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kusaini makubaliano vijana wa Temeke kupata mafunzo kwa ufadhili wa jeshi la Wokovu hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.