Sunday, August 25

DC LYANIVA AAHIDI KUTATUA KERO ZA WAFANYABISHARA TANDIKA

0


Na Zainab Nyamka, Globu ya jamii
MKUU wa Wilaya ya Temeke Dar es Salaam  Felix Lyaniva amekutana na wafanyabiashara wa Tandika ambapo amewaahidi kuhakikisha anatatua kero ambazo zinawakabili kwenye biashara zao. 

Ametoa aahadi hiyo leo wilayani Temeke akiwa katika ziara yake ya kutembelea maeneo yanayotoa huduma za jamii katika wilaya ya Temeke ambapo amewaambia wafanyabiashara hao kuwa ataondoa kero zote zinazolikumba soko hilo .

Moja ya kero kubwa inayoikumba soko hilo ni miundombinu inayoizunguka soko hilo, ikiwemo kutuama kwa maji kipindi cha mvua ambapo Lyaniva amewaahidi wafanyabishara kushughulikia kero hizo ili kuhakikisha mahali hapo panakua salama kwaajili ya kutoa huduma za kijamii.

Katika ziara hiyo aliambatana na katibu Tawala wilaya,watumishi kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke,diwani wa Tandika,wenyeviti wa Mitaa,wakuu wa vyama vya siasa mbalimbali,wajumbe wa Mitaa,ofisa Tarafa Chang’ombe na wadau wa utoaji huduma za jamii mbalimbali ikiwemo TARURA,TAKUKURU,DAWASCO na TRA.

Katika hatua nyingine mkuu wa wilaya ameenda katika Ofisi ya kata ya Tandika ambapo alifanya kikao cha wadau wa maendeleo na wananchi. Akiwa hapo amesisitiza kuhakikisha wanafunzi wote waliofauru darasa la saba 2017 kama wameripoti shuleni.

Amewataka wazazi kutoa ushirikiano ili watoto wao wasibaki nyumbani kujiingiza katika makundi hatarishi.

Hata hivyo Lyaniva aliwataka wananchi kutoa kiwango stahiki cha kuzoa takataka ili kusaidia zoezi la ukusanyaji taka kuwa rahisi. 

Pia alisisitiza usafi wa kila jumamosi kwa wananchi wote ni lazima.
Pia aliwataka wananchi kuchangamkia fursa ya mikopo ya jamii inayotolewa na serikali kwa riba nafuu kupitia benki ya DCB. 

Wakinamama na vijana wamehamasishwa kwenda kuchangamkia fursa hiyo ili kujikwamua katika hali ya kiuchumi na jamii.

Lyaniva alisisitiza kuwa rushwa ni adui wa haki hivyo endapo mwananchi atakutana na mazingira yoyote ya rushwa atoe taarifa katika ofisi za TAKUKURU Wilaya ili hatua kali za kisheria zichukuliwe. 

Amesema huduma za jamii ni bure kwa kila mtu hivyo wananchi wasiruhusu vitendo vya rushwa na kuwataka wananchi kulipa kodi na tozo mbalimbali zinazotolewa na Halmashauri ili kuiongezea mapato Serikali,na kwa mapato hayo hayo yatasaidia kuboresha huduma za jamii. 

Ziara hiyo ya mkuu wa wilaya yenye lengo la kusikiliza na kutatua changamoto zilizopo katika jamii itaendelea katika kata zote zilizopo wilaya ya Temeke katika vipindi tofauti tofauti.
 Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva akizungumza na wafanyabiashara wa soko la Tandika ambapo amewaahidi kuhakikisha anatatua kero ambazo zinawakabili kwenye biashara zao
Baadhi ya wafanyabiashara wa soko la TandikaRead More

Share.

About Author

Comments are closed.