Monday, August 19

BODABODA KUANZA KUTUMIKA KUSAFIRISHA MAKOZI YA TB

0


*Ummy Mwalimu azindua dawa ya TB kwa watoto,aagiza wanafunzi nao kupimwa ugonjwa huo 

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema wapo kwenye mchakato wa kuingia mkataba na waendesha bodaboda ili watumike kusafirisha makozi ya Kifua Kikuu(TB) kutoka vituo vya afya kwenda Hospitali kwa ajili ya vipimo.

Pia amezindua rasmi dawa ya TB kwa ajili ya watoto wenye kubainika kuwa na ugojwa huo ambayo ni tamu na ina ladha ya matunda huku akisisitiza umuhimu wa kila mmoja wetu kupambana kutokomeza TB kwani ni janga la kitaifa.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa watalaam na wadau wa afya na hasa katika ugonjwa wa TB, Waziri Ummy Mwalimu amesema ugonjwa huo ni tishio nchini na duniani kwa ujumla.

Hivyo amesema kuna jitihada mbalimbali ambazo zinafanywa na  Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya  Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Amesema licha ya kufanikiwa kuwatambua wagonjwa wa TB lakini changamoto kubwa bado wengi wao wanajificha.Hivyo inakuwa ngumu kutambua na ubaya wake TB inaambukizwa kwa hewa.
Amesema takwimu zinaonesha mgonjwa wa TB anaweza kuambukiza watu wengine 20, hivyo kazi inayofanyika sasa ni kuendelea kuelimisha jamii kupima ili kubaini iwapo wana TB au laa.

Pia amesema kutokana na uhaba wa vifaa vya kupima wenye ugonjwa wa TB inalazimu kwenye vitio vya afya baada ya kuchukua makozi ya mtu anayedhaniwa kuwa na ugonjwa huo husafirishwa kwa gari hadi hospitalini.

Hata hivyo amesema kuna changamoto katika eneo hilo na mchakato unaondelea ni kuingia makubaliano na waendesha bodaboda ambao watakuwa wakifuata makohozi hayo vituo vya afya na kisha kuvipeleka hospitalini.

“Tunao mkakati wa kuwatumia waendesha bodaboda na hasa maeneo ya vijijini kwa kuingia nao mkataba na tutawalipa fedha.Watakuwa wakichukua makozi yanayotakiwa kupimwa kutoka vituo vya afya na kuvipeleka katika hospitali.

“Lengo letu ni kuhakikisha tunatokomeza TB nchini kwani , kwa mwaka takwimu zinaonesha idadi ya wanaobainika kuwa na TB ni watu 160,000 na kati yao asilimia 10 ni watoto,”amesma Waziri Mwalimu.

AZINDUA DAWA YA TB YA WATOTO
Wakati huohuo, Waziri Mwalim amezindua dawa ya TB ambayo itatumika kwa watoto watakaobainika kuwa na ugonjwa huo.

Amesema tayari dawa hiyo imesambazwa katika hospitali na vituo vya afya nchini na sasa mtoto mwenye TB atatumia dawa halisi kwa ajili yake tofauti na zamani ambapo mtoto mwenye TB amekuwa akipewa dawa za mtu mzima mwenye ugonjwa huo.

AAGIZA WANAFUNZI KUPIMWA TB 
Pia ameagiza kuwa kuanzia sasa mwanafunzi kabla ya kuanza shule apimwe ili kubainika kama ana TB aanze matibabu.

Amesema maagizo hayo yaanze mara moja na kushauri wazazi kujenga utamaduni wa kupima watoto afya zao na kwenye fomu za shule ambazo mwanafunzi anatakiwa kuzijaza lazima awe amepima na kuonesha vithibitisho.”Hivyo hata wale wanaokwenda shule za bweni nao lazima wapimwe TB.Tunataka kupunguza kasi ya maambukizi.”

WAGANGA TIBA ASILI WAOMBWA USHIRIKIANO
Wakati huohuo, Ummy Mwalimu amesema Serikali inatambua mchango wa waganga wa tiba asili, lakini amewaomba ni vema wakashiriki katika kukomesha TB kwa kuhakikisha wale wagonjwa ambao wanakwenda kwao kwa ajili tiba basi wawashauri waende na hosptali kupima afya.

“Mganga wa tiba asili huna sababu ya kukaa na mgonjwa kwenye kilinge chako wakati unaona muda mwingi anakohoa.Ni vema ukamshauri aende hospitali kupima badala ya kuendelea kukaa naye,”amesema.

Pia leo amekabidhi mashine tano za Genexpert ambazo ni maalumu kupima makozi yanayodhaniwa kuwa na TB.

Amekabidhi mashine hizo kwa baadhi ya hospitali ambazo zimekuwa zikishirikiana na Serikali katika kupambana na TB nchini ambapo thamani kwa kila mashine moja na Sh.milioni 34.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akizungungumza wakati wa mkutano wa wadau wa afya waliokuwa wanajadili namna ya kutokomeza Kifua Kikuu(TB) ambapo ametumia mkutano huo kuzindua dawa ya TB kwa watoto waliobainika na watakaobainika kuwa na ugonjwa huo leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akitoa ufafanuzi kabla ya kumpatia dawa ya TB mtoto Salome Makulusi(3) aliyebainika kuwa na ugonjwa huo.Waziri Mwalim amesema dawa ya TB tayari imeingia nchini na leo ameizundua rasmi wa kwanza kushoto ni Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Muhammed Bakari Kambi.
 Baadhi ya wadau wa afya hasa wanaojihusisha na tiba ya ugonjwa wa TB wakimsikiliza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto leo jijini Dar es Salaam.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.