Saturday, August 24

ASKARI POLISI AELEZA NAMNA ALIVYOPIGWA JIWE WAKATI AKIZUIA MAANDAMANO YA WAFUASI WA CHADEMA

0ASKARI Polisi namba H 7856  PC Fikiri Mgeta (28), ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa alilazwa siku tatu katika Hospitali ya Polisi Kilwa road, baada ya kupigwa jiwe kichwani wakati akizuia wa maandamano ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Mgeta anayefanya kazi Kituo cha Polisi Oysterbay anakuwa shahidi wa nne katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi hao akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Jacqueline Nyantori, shahidi huyo akiwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amedai kuwa alipigwa na jiwe kichwani pamoja na mkononi ambayo yalimuumiza na kusababisha kutoka damu nyingi.

Mgeta amedai kuwa tukio hilo lilitokea Februari 16, mwaka jana wakati walipokwenda kutuliza waandamanaji waliokuwa wamebeba mawe, chupa na fimbo eneo la Mkwajuni wilaya ya Kinondoni.

Shahidi huyo amedai kuwa chanzo cha kupigwa na mawe ni baada ya waandamanaji hao wakiongozwa na Mbowe kutotii ilani iliyotolewa na Ofisa Operesheni wa Polisi  sambamba na mabomu ya machozi yaliyopigwa.

“Afande Ngiichi aliagiza mabomu yatumike kutuliza waandamanaji lakini muitikio ulikuwa hasi kwani waliendelea kusonga mbele kuwafuata askari huku wakiimba na kurusha mawe,” amedai Mgeta.

Shahidi huyo alidai mawe yalirushwa zaidi upande wa askari na ndipo mmoja wa askari Koplo Rahimu alipigwa na jiwe  na kuanguka chini huku akidai kuwa baada ya kuanguka alilalamika  ameumizwa upande wa shingo na kupoteza fahamu.

“Afande alitoa amri tumsaidie mwenzetu hivyo nikiwa katika kumsaidia nilipigwa na jiwe  mkono wa kulia na nilipoteza saa, nikiwa katika hamaki nilipigwa tena na jiwe kichwani ambalo liliniumiza hadi nilisikia kizunguzungu,” alieleza.

Pia amedai kuwa hakuweza kuendelea na kazi yake kwani alichukuliwa na askari mwenzake na kumpeleka kwenye gari  na kupelekwa hospitali ya Polisi Kilwa Road kwa ajili ya matibabu zaidi.

Mgeta amedai kuwa alifika hospitalini hapo majira ya saa 1 kwenda saa 2 usiku akiwa na fomu namba tatu ya polisi (PF 3), na kuanza kupatiwa huduma ya kwanza.

Mgeta ameieleza mahakama kuwa alilazwa hospitalini hapo kwa siku tatu kuanzia Februari 16 hadi 18, mwaka jana ndipo saa 10 jioni ya siku hiyo daktari alimruhusu kwenda mapumziko ya wiki mbili nyumbani.

Hata hivyo, shahidi ameiomba mahakama kupokea PF3 hiyo ili itumike kama kielelezo na upande wa utetezi haukuwa na pingamizi.

Akielezea tukio hilo, Mgeta amedai kuwa aliajiriwa na Jeshi la Polisi mwaka 2015 baada ya kupata mafunzo kutoka Chuo cha Polisi Moshi.

Amedai siku ya tukio alipangiwa kufanya doria eneo la Mwananyamala na majira ya jioni walipewa taarifa na kiongozi wao kuwa kuna mkusanyiko wa watu unaoashiria uvunjifu wa amani.

“Tuliitikia wito na tukaelekea tulipoelekezwa eneo la Mkwajuni ambako tulikuta viongozi na wafuasi wa Chadema wakiwa zaidi ya 500 wamefunga barabara huku wakiwa na uhamasishaji kwa njia ya nyimbo hali iliyoashiria kuvunja amani,” alidai Mgeta.

Shahidi huyo amedai kuwa wakiwa wanatumia gari la Polisi walipita kwa shida katikati ya maandamano hayo na walikuta ilani inatamkwa huku ikitaja jina la Rais John Magufuli.

Mgeta  amedai  kuwa mkusanyiko huo ukiongozwa na viongozi wa Chadema ambao alidai wengine anawafahamu kwa majina na sura huku wengine akiwafahamu kwa sura pekee,  haukutii amri iliyokuwa inatolewa.

shahidi huyo amedai kuwa aliwatambua baadhi ya viongozi hao kupitia kwenye shughuli mbalimbali za kisiasa ikiwemo kampeni na Bungeni.

Mgeta  amedai kuwa viongozi hao waliendelea kuhamasisha kwa ishara ya mikono kwa kuwahimiza wafuasi wasonge mbele kuwafuata askari na walikuwa wakirusha mawe.

Mbali ya Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Katibu Mkuu Taifa, Dk Vincent Mashinji ,  Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Taifa, Zanzibar, Salum Mwalimu,  Mbunge wa Kibamba, John Mnyika,  Katibu Mkuu Taifa, Vicent Mashinji,  Mbunge wa Kawe,  Halima Mdee,  Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko na Mbunge wa Bunda,  Ester Bulaya.

Share.

About Author

Leave A Reply