Saturday, August 24

Wauza Kahawa kwa magendo kukamatwa

0


Ngara. Kamati za ulinzi na usalama za wilaya zote mkoani Kagera zimeagizwa kuwasaka na kuwakamata watu wanaouza kahawa nje ya nchi kwa magendo.

Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba pia ameviagiza vyombo vya dola viwashughulikie watakaonunua kahawa ikiwa changa mashambani kwa sababu kufanya hivyo ni kuwanyonya wakulima wa zao hilo.

Dk Tizeba alitoa maagizo hayo jana baada ya ziara ya kikazi mkoani Kagera wakati akizungumza na uongozi wa Chama cha Wakulima Ngara na wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara.

Alisema ni marufuku wakulima kuuza kahawa kwa walanguzi na kwamba yote itanunuliwa na vyama vya ushirika ambavyo vitaipeleka katika mnada na kununuliwa na kampuni zitakazojitokeza kwa kushindanisha bei katika soko la dunia na ubora wake kati ya arabika na robusta.

“Naagiza na kupiga marufuku kuvuna, kununua na kuuza kahawa mbichi yaani ‘butula’ na kamati za ulinzi na usalama za kila eneo la utawala zisimamie agizo hili kulinda haki ya mkulima anayehujumiwa na walanguzi,” alisema.

Alisema Serikali imeandaa utaratibu wa kushindanisha kampuni kununua kahawa mnadani baada ya wakulima kuviuzia vyama vya ushirika na kulipwa fedha taslimu huku wakisubiri nyongeza kutokana na faida itakayopatikana.

Akizungumza katika kikao hicho, mkurugenzi wa kampuni ya Arab Glob ya mjini Ngara, Abdallah Seif ambaye alikuwa akinunua kahawa kutoka kwa wakulima, alisema atashirikiana na Serikali kununua zao hilo kwenye minada.

Alisema alikuwa akinunua kahawa kutoka kwa wakulima kwa kutumia mawakala ili kuzuia kahawa ya Ngara kuuzwa nchini Burundi, baada ya Chama cha Wakulima cha Ngara kufilisika na wakulima kuuza zao hilo kwa magendo.Read More

Share.

Comments are closed.