Saturday, July 20

Watoto wawili wateketea kwa moto wakiwa wamelala

0
Na John Walter-Hanang

Watoto  wawili wamefariki dunia baada ya nyumba waliyokuwa wamelala kushika  moto na kuteketea katika kijiji cha Nyabati wilayani Hanang Mkoa wa Manyara.

Katika tukio hilo pia wamekufa Kondoo wawili [2], Mbuzi nane [8], Kuku kumi [10],Mahindi gunia kumi [10] na piki piki aina ya Honda huku thamani ya mali zote zilizoungua zikiwa bado hazijafahamika.

Kamanda wa polisi mkoa wa Manyara [SACP] Agustino Senga Amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo ameeleza kuwa limetokea Novemba 7.2018  majira ya saa saba usiku katika eneo la Bassoutu Hanang.

Kamanda Senga aliiambia Muungwana Blog kuwa moto uliochoma nyumba hiyo iliyokuwa imeezekwa kwa nyasi uliwashwa ili kuleta joto katika kipindi hiki cha baridi maeneo hayo ndipo ulipowazidi na kushika nyasi za ukutani na kusababisha vifo vya  watoto hao Raheli Peter [12]  na  Agatha Israel [12] ambao ni wanafunzi wa shule ya msingi katika eneo la Bassoutu.

Alisema Nyumba iliyoungua kupelekea vifo hivyo, inamilikiwa na Bwana Petro Lagwen mwenye umri wa miaka 48  ambaye kazi yake ni mkulima.

Kamanda Senga alisema wazazi wa watoto hao wanaishi nyumba nyingine tofauti,hivyo kwa usiku huo baada ya kuzidiwa walikosa msaada.

Alisema “sio vizuri kuwaacha watoto wadogo wakalala peke yao,  ingekuwa vizuri wakalala na watu wazima na mara nyingine tuchukue  tahadhari katika moto kama hii,isingekuwa vizuri kuacha moto usiku bila kuwa na uangalizi wa watu wazima ili kuondokana na Madhara ya namna hii”.


Share.

Leave A Reply