Sunday, August 18

Wanasiasa nane washukiwa vikali na RC Mnyeti

0


Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amewashukia vikali wanasiasa nane wa Kata ya Kitwai Wilayani Simanjiro wanaorudisha nyuma maendeleo kwa kukataza wanafunzi wasisome kwenye madarasa ya shule ya msingi Kitwai B yaliyojengwa na mdau wa maendeleo hivyo kuyasusia.

Akizungumza wakati akizindua madarasa matatu mapya ya shule hiyo, Mnyeti alisema wanasiasa hao atawachukulia hatua kali wanaoshawishi wananchi kususia maendeleo.

Alisema hatakubali kuona watu wachache wanaopinga maendeleo, hivyo serikali itamuunga mkono mdau huyo wa maendeleo Sanare Mollel ambaye pia ana mpango wa kumalizia majengo ya zahanati ya kijiji hicho.

“Wanasiasa hao wanampinga mdau huyo kwa sababu ni mfugaji mkubwa ambaye amefuata taratibu na kanuni zote za kuingia ndani ya kijiji hicho lakini hajavunja sheria kwani mtanzania anaruhusiwa kuishi popote,” alisema Mnyeti.

RC Mnyeti alisema haiwezekani mdau wa maendeleo Sanare Mollel ajitolee kujenga madarasa matatu kisha baadhi ya wanasiasa wanawaambia wananchi wasisomeshe watoto.

Diwani wa kata hiyo Nyika Shawishi alisema wapinzani wake wa kisiasa ndiyo wanaosababisha hali hiyo kwani wanaona maendeleo yakifanyika sifa zitakuwa kwake.

“Maboma matano yanayoongozwa na viongozi niliowashinda kwenye uchaguzi uliopita ndiyo wanasababisha uchochezi wa kugomea maendeleo,” alisema Shawishi.


Share.

Leave A Reply