Monday, August 19

Japan yaridhishwa na matumizi ya fedha zao nchini

0


Balozi wa Japan nchini, Shinichi Goto amesema serikali ya nchi yake inaridhishwa na matumizi ya fedha za msaada wanazotoa kupitia mashirika mbalimbali kwa ajili ya kuchangia utetekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya afya, elimu na miundombinu.

Akiwa mwakilishi wa Japana nchini, Goto alisema ataendelea kuisemea Tanzania kwa nchi wahisani ili iendelee kusaidiwa pamoja na kuwashawishi wawekezaji kutoka Japan kuja kuwekeza katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

Aliyasema hayo kwenye sherehe za kuadhimisha miaka 10 ya Kituo cha Kulea Watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha Amani Orphans Home cha Mbigili wilayani Kilolo, mkoani Iringa. Kwa kupitia ubalozi huo, Serikali ya Japan ilikisaidia kituo hicho kwa kukipatia msaada wa Dola za Marekani zaidi ya 80,000 zilizotumika kujenga majengo matatu ya kuishi watoto hao.

“Tumeridhishwa na matumizi ya msaada huo katika kituo hiki, ni matarajio yetu kitaendelea kutoa huduma zake kwa ufanisi mkubwa zaidi,” alisema.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi aliyeambatana na balozi huyo na viongozi wengine wa mkoa wake alizielekeza halmashauri za wilaya mkoani humo kuweka mipango ya namna ya kuwasaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi ili kuwanusuru.

Hapi alisema kama ilivyo kwa watoto wengine, watoto walio katika mazingira hayo wana haki ya kuishi, kuendelezwa na kufurahia maisha yao ya sasa na baadae hivyo ni wajibu jamii inayowazunguka ikajiwekea utaratibu wa kuwasaidia. “Mwanzilishi wa kituo hiki ni mjerumani, na katika kituo hiki kuna wafanyakazi wa kujitolea kutoka Ujerumani, hawa watu wametoka mbali sana kuja kushughulikia matatizo yetu.

Watoto hawa ni watanzania wenzetu, na sisi tujenge utamaduni wa kujitolea kuwahudumia,” alisema. Katika taarifa yake, mwenyekiti wa bodi ya kituo hicho, Gabriel Chuwa alisema lengo la kuazishwa kwa kituo hicho ni kuwawezesha Watoto yatima na wanaoishi mazingira magumu kupata fursa za elimu na huduma za afya kama walivyo watoto wengine.

Alisema tangu kuanzishwa kwake miaka 10 iliyopita, kituo hicho kimewawezesha watoto zaidi ya 300 walio katika mazingira hayo kupata fursa hizo. “Kati yao wapo waliotimiza ndoto zao kwa kupata elimu ya chuo kikuu, wanayoitumia kwasasa kuendeleza maisha yao na familia zao,”alisema.

Akizungumza kwa niaba ya mwanzilishi wa kituo hicho, Luisa Tersteegen aliipongeza Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na kitengo cha ustawi wa jamii kwa kutoa usajili wa kituo hicho.


Share.

Leave A Reply