Sunday, August 18

Askofu Pengo awataka wananchi wasiogope kutekeleza majukumu yao

0


Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amewataka wananchi wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya wasiogope kutekeleza majukumu yao.

Kardinali Pengo ametoa wito huo leo Jumapili Aprili 28, 2019 wakati wa mahubiri kwenye misa ya kumsimika askofu wa kwanza Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya, Gervas Nyaisonga inayofanyika katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya na kurushwa moja kwa moja na TBC.

“Wana Jimbo Kuu jipya la Mbeya msiogope, pokeeni wajibu wenu, tekelezeni majukumu yenu, amesema Kardinali Pengo na kuhoji: “Lakini ni jambo gani ambalo litawapa ujasiri kiasi kwamba mkaacha kuogopa na mkatenda shughuli zenu kwa ujasiri ule unaotakiwa? Ni maneno ya aliyoyasema Bwana wetu Yesu Kristo katika injili ya leo, alipowavuvia wanafunzi wake, aliwaambia pokeeni Roho Mtakatifu” amesema Kardinali Pengo akirejea injili iliyosomwa katika misa hiyo.

“Kazi yenu kuu chini ya uongozi wa askofu wetu mkuu (Gervas Nyaisonga) ni kuondoa dhambi, lakini hiyo ifanyike chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, mpokeeni Roho Mtakatifu, huyu ndiye atakayewasaidia kutekeleza wajibu mlioupokea leo,” amesema.

Misa ya kusimikwa askofu wa kwanza mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya, Gervas Nyaisonga ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maskofu Katoliki Tanzania (TEC) imehudhuriwa na maaskofu wa majimbo mbalimbali nchini, Balozi wa Baba Mtakatifu nchini, Askofu Mkuu Marek Solczynski.

Pia, misa hiyo imehudhuriwa na Rais John Magufuli, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, mawaziri na manaibu waziri na viongozi mbalimbali.


Share.

Leave A Reply