Friday, May 24

Maandalizi ndio silaha kubwa ya kumridhisha mpenzi wako

0KARIBU jamvini mpenzi msomaji kwa kuwa Mungu ametujalia siha njema na tumekutana tena leo kwa mapenzi yake. Nalazimika kuileta mada hii kwa mara nyingine baada ya kupokea malalamiko mengi juu ya wenza kushindwa kuandaana wakati wa ‘chakula cha usiku’ (tendo la ndoa).

Ukweli ni kwamba ‘maandalizi’ ndiyo kila kitu kwenye tendo. Unapotaka kitu chochote kiwe na mafanikio maandalizi ya uhakika ni lazima. Iwe kuoa, kuchumbia, kupika, kulima, kujenga, kufua, kufaulu, kununua nyumba, gari au kitu chochote, maandalizi hayaepukiki na hapa hakuna kulipualipua au ‘zima moto’.

Maandalizi ni jambo linalohitaji utulivu wa hali ya juu na hasa kwenye mapenzi unapojilia vyako ambavyo siyo vya wizi. Unapotaka kufanya jambo lolote linahitaji maandalizi ili kulifanya kuwa sahihi na lenye ubora wa hali ya juu.

Maandalizi husaidia kurahisisha jambo husika kulifanya kwa urahisi tofauti na mtu ambaye hajafanya maandalizi. Si kazi ngumu pekee zinazohitaji maandalizi. La hasha! Hata kazi ya kukutana faragha na mwenza wako nayo inahitaji maandalizi kabambe na tena siyo lelemama kama yafuatayo;

KIAIKILI/KISAIKOLOJIA
Kwa watu wanaopendana ni lazima watakuwa na maelewano hivyo kabla ya kukutana faragha, lazima watu hawa watakuwa na mawasiliano na maridhiano kwa ajili ya faragha.

Hivyo, hata unapofika muda wa wapenzi hawa kukutana kwenye dimbwi la mahaba, basi kila mtu anakuwa ameridhia, kimwili, kisaikolojia na hata akili yake inakuwa inafahamu nini kitaendelea muda f’lani na sehemu f’lani. Lakini kama hamtakuwa na maelewano na maridhiano katika penzi au ndoa yenu, hata muda wa tendo au faragha yenu haitakuwa na utamu wowote kwa sababu akili ya mhitaji imejiandaa, lakini ya mhitajiwa haijaandaliwa.

Kwa mantiki hiyo, kinachokwenda kufanyika ni kulazimisha na mara nyingi tabia hii hutumiwa sana na wanaume na ndipo hapo kama mwanaume atalazimisha na mwanamke akakataa, basi nguvu hutumika na mwisho wa siku hutafsiriwa kuwa mwanaume amembaka mkewe na hii ni kesi nzito. Unadhani kwa kulazimisha na kukurupushana kushiriki tendo la ndoa kunaweza kuwafanya wote mkafurahia kweli kama siyo kuifanya faragha yenu kuwa ni karaha?


Share.

Leave A Reply