Friday, March 22

Kama kupenda kwako ni hivi, Tayari umeshapotea

0



Msichana mdogo wa miaka 18 aliwahi kuja kwangu na kuniomba msaada. Hakuhitaji msaada mkubwa sana kama mwenyewe alivyosema, kwani alitaka kusaidiwa kupata jibu la swali ambalo lilikuwa likimtatiza kwa muda mrefu.

“Nataka kujua maana ya kupenda.” ilikuwa ndiyo kauli yake, fupi na inayoeleweka. Sikujibu swali lake moja kwa moja bali nilimwambia, ”umesema unahitaji msaada mdogo, lakini unayemwomba hana uwezo wa kukusaidia.” Nilizidi kumwambia kwamba, hata mimi nimekuwa kwa muda mrefu nikitafuta jibu la swali hilohilo.

Hivyo, sikuweza kumsaidia na niliona jambo lile lilinipa changamoto nami kuanza kusaka jibu la swali lile. Lakini, bahati nzuri ni kwamba, kabla yule msichana hajaondoka kwangu nilimuuliza nami swali moja. “Ni kwa nini unataka kujua maana ya kupenda”?

Alinijibu bila kufikiri mara mbili kwamba, ni kwa sababu gani anataka kujua kama mpenzi wake anampenda. Pengine jibu lake lilinizindua na nilihisi kama vile ndani ya jibu hilo kungeweza kupatikana pia jibu la lile swali lake. ”Ukishajua kama anakupenda ndiyo itakuwa nini baada ya hapo?” Nilimuuliza, pengine nikiwa sitegemei jibu.

Alikuwa ni msichana ambaye majibu yake yameandaliwa tayari kutolewa. ”si ndiyo nijue hanidanganyi, sasa nitampenda vipi kama yeye hanipendi!” alipomaliza kunijibu, nami nikawa nimepata jibu la swali lake.

Wengi husubiri kupendwa kwanza, siyo msichana yule tu, bali wengi miongoni mwetu tunasubiri kupendwa au huwa tunataka kwanza kuwa na uhakika kuwa tunapendwa, ndipo nasi tupende.

Penda kwanza, kabla hujapendwa.

Ukimfuata mtu na kumwambia kuwa unampenda, ungependa awe mpenzi wako au mwezi wa baadaye maishani na mtu huyu akawa mkweli na kukuambia kwamba, yeye hakupendi, utaumia sana. Utaanza hapohapo kumchukia au hata kumfanyia visa.

Unakuwa katika hali hiyo kwa sababu kuu mbili. Kwanza, ni kwa sababu hujui kwamba, kinyume cha kupenda siyo kuchukia. Unapomtaka mtu uhusiano na akasema hapana, unamchukulia kuwa anakuchukia kwa sababu, kwako kama hakuna kupenda, basi ni lazima kuwe na kuchukia.

Tumelelewa na kukulia katika mazingira ambayo yametufundisha kukitazama kila kitu katika uwili. Kwa hiyo, `sikupendi`masikioni mwetu inasikika kama, `nakuchukia`. Pili, ambavyo ni kubwa, ni kwa sababu kila binadamu anahitaji kupendwa. Wataalamu wengi wa saikolojia wanabainisha kupendwa kama moja ya mahitaji muhimu kwenye ngazi ya mahitaji ya binadamu.

Tangu tukiwa na umri wa siku moja, tunataka kukubaliwa kupokelewa na kulindwa. Haya ya kupendwa ni kama jambo la kimaumbile kwa binadamu. Unapogundua kuwa watu wote hawakupendi ni lazima utababaika, utachanganyikiwa na kwako maisha yanaweza kupoteza maana.
Wengi tunafanya tuyofanya au kuacha kufanya katika kutafuta kupendwa. Kwa hiyo, kila mmoja wetu ana kiu kubwa ya kupendwa. Hapa ndipo linapochipuka tatizo kubwa linalofanya wengi kushindwa kujibu swali la , `kupenda ni nini?`

Hushindwa kwa sababu, hakuna anayejali kupenda, karibu wote tunajali kupendwa, tuna kiu ya kupendwa, siyo kupenda. Kama nguvu zetu zote tumeziweka kwenye kupendwa, kupenda kunakuwa na nafasi gani kwetu? Ndiyo maana wengi hatuju kupenda ni nini?

Ni kitu gani kinatokea? Ni kwamba, badala ya kuwekeza kwenye kupenda, tunawekeza kwenye kupendwa ambako hakutuhusu. Ni sawa na mtu kuchukua fedha zake na kuziingiza kwenye akaunti ya mwingine akiamini kwamba anaziingiza kwanye akaunti yake. Siku anapokuja kutaka kutoa fedha na kukuta hazipo atazusha zogo kubwa na balaa lisilowezekana. Atadai kwamba benki hazifai na hazina ukweli.

Unaposubiri au kutarajia na mbaya zaidi kudai kupendwa, unapoteza muda wako bure, kwa sababu hilo ni jambo lisilokuhusu. Ni jambo ambalo huwezi kulipanga wala kulidhibiti kwa sababu linamhusu mtu wa upande wa pili. Inawezeakana vipi wewe umalazimishe mtu akupende? Haiwezekani, lakini tunafanya. Tunafanya lisilowezekana.
Lakini unaweza kupenda, kwani ni jambo linalotoka kwako , lililo ndani ya uwezo wako. Kwa hiyo, unapokutana na mtu, kama amekuvutia, wewe ndiye unayetakiwa kumpa upendo, bila kujali kama naye anakufanyia hivyo. Huna haja ya kujali kama naye anakufanyia hivyo kwa sababu, wewe umeamua kumpenda, lakini huna haki na huwezi kumfanya akupende kama yeye hataki.

Bila shaka huwa unakutana na vituko vya karne kila siku kuhusu jambo hili. Mtu anaambiwa na mwingine kwamba hampendi. Inawezekana kuwa ni wapenzi wa muda mrefu-mke na mume au hata wa muda mfupi.

Badala ya huyu anayeambiwa hapendwi kukubali jambo hilo kwa sababu hawezi kulibadili, huanza kupinga. Wengine huenda hata mahakamani au kuwauwa wapenzi waliowakataa, ni kweli hii?
Vituko hivi viko hata katika mazingira ambapo hakuna ugomvi au kutoelewana. Inawezekana ni katika mazingira ya kawaida kabisa, ambapo mpenzi anamuuliza mwenzake , ”hivi, unanipenda kweli, hebu nithibitishie”.

Shabashi! Ni kitu gani hiki! Tangu lini kupendwa limekuwa ni jukumu lako? Jukumu lako ni kupenda, basi. Hili jukumu la kupendwa muachie mwingine. Kupenda ni hisia na ndiyo maana imekuwa vigumu sana kwa watu kumudu kusema mapenzi ni nini.

Jambo loloto la kuhisi ni gumu kuelezewa kwa maneno. Kupenda kunapoelezeka kwamba ni kitu fulani, ni lazima kuna mushkeli. Watu wengi ambao huwa ninazungumza nao katika kushauriana au kufundishana kuhusu kupenda, huwa ninawauliza swali hili ”Umempendae kitu gani mwenzako?” Wengi huwa wanatoa maelezo kama vile, ”nimempendea upole wake” au ”nimempenddea ukarimu wake” ama ”nimempendea tabia zake”.

Lakini hakuna kabisa ambao wamewahi kusema wamempenda mwingine kwa sababu ya sura au maumbile yao au kwa sababu ya utajiri ama umaarufu wao . Kwa nini?

Ni kwa sababu, ndani ya nafsi zetu tunajua kwamba kupenda sifa za nje ni jambo linalopingwa na kila mtu na ni aibu kulitamka, labda tu miongoni mwa watu waliozoeana sana na kuaminiana.
Hata hivyo, miongoni mwa wapenzi, jambo hilo huwa linasemwa sana bila wenyewe kungámua. ”Unaniacha hoi kwa macho yako,” ni kauli za kawaida kwa wapenzi. Kusikia mpenzi akimwambia mwingine ”nimekupenda kwa kweli, guu unalo,” ni jambo la kawaida.

Mwanamke na kuita hali hiyo kuwa ni kupenda. Hutamani sana sura, miguu, matiti, makalio, macho na hata midomo na pua. Hili ni jambo la kimaumbile zaidi. Ndiyo maana wanawake wanajipamba na kujikwatua. Hufanya hivyo ili kuwavuta wanaume, kwani wanaume hujali muonekano wa nje zaidi.

Kuna wakati hapa nchini suala la wanawake kubabua ngozi au kupaka dawa nywele zao lilikuwa ni suala la mjadala mkubwa. Baadhi ya wanawake ambao walitakiwa kutoa maoni yao kuhusu jambo hili walisema, wao hawapendi sana kufanya hivyo, bali wanaume ndiyo wanaowalazimisha kufanya hivyo.
”Mwanaume anaweza kukuacha kwa sababu tu kaona mwingine mwenye ngozi nyeupe na nyororo au nywele laini zilizoangukia mabegani. Inabidi ujitahidi kumlinda.” walisema baadhi ya wanawake. Pamoja na kuwa ni kauli zenye kuonyesha unyonge, lakini zina ukweli. Wanaume hukimbilia sifa za nje zaidi.

Wanawake kwa upande wao, huvutwa zaidi na wanaume ambao wanaweza kuwalinda au kuwapa uhakika fulani wa kimaisha. Hata hivyo, unapowauliza kwa nini wamempenda fulani, nao hawawezi kusema ni kwa sababu ana fedha au kwa sababu ana jina, hapana. Ni aibu kukiri hivyo au pia kwa sehemu kubwa huwa hawajui kwamba wamevutwa na sifa hizo.

Ni wachache sana ambao hutokea wakajibu kwamba wamempenda mwingine kwa kumpenda tu, bila kutoa maelezo. Kwa nini ni wachache? Ni kwa sababu, wanaopenda siyo wengi. Mtu anayesema nimempenda fulani bila kujua ni kwa nini hasa, huyu ndiye ambaye amependa. Huku ndiko tunakoita kupenda tunapopenda, kwa kawaida kuwa hatujui sababu za kumpenda huyo fulani, bali tunampenda tu. Mtu anapotoa sababu ya kumpenda mwingine, huyo hajapenda bado. Huu ndiyo ukweli!

Kwa bahati mbaya, kuna wengine wamependa na hawajui ni kwa nini wamependa. Lakini unapowauliza, wanaanza kujaribu kutafuta sababu za huko kupenda kwako. Kwa hiyo, mtu ataanza kusema, `nampendea upole`au `nampendea huruma zake` ama `nampenda kwa sabu ametulia.” Anasema haya kwa sababu anaamini kwamba, kupenda ni lazima kutolewe sababu, wakati kinyume chake ndiyo ukweli.

Unapovutwa na mtu na ukajikuta huna sababu unazoweza kuzitoa za kwa nini umevutwa naye, kuna uwezekano mkubwa kwamba uko kwenye upendo wa kweli na mtu huyo. Lakini pale ambapo unaziona sababu waziwazi za kumpenda kwako, hapo hakuna upendo wa kweli.

Kumbuka kuwa sababu zote unazoziona ni za muda, zinaweza kuondoka. Zinapoondoka, ina maana pia kwamba, upendo haupo. Kama ulimpenda kwa sababu ya tabia ya upole na ukarimu, anapokuja kubadilika na kuiacha tabia hiyo, itakuwa na maana pia kwamba, mapenzi hayatakuwepo kwani ulichokipenda kitakuwa hakipo.

Lakini ukiona mwingine mwenye upole na ukarimu kuliko huyo, utampenda zaidi pia. Je, utaacha kumpenda yule wa kwanza au utawapanga kwa madaraja kiupendo?

Kama ulimpendea sura, mguu au jicho, ni wazi upendo wenu utakuwa ni wa muda kwani kwa kadiri siku zinavyopita, vitu hivyo havyo hupoteza nuru na mvuto. Mazoea nayo huingiza ukinaifu wa hisia. Lakini kuna wengine ambao wana miguu na macho mazuri zaidi ya hayo ya huyo. Hii ina maana kwamba, utahama kutoka mtu mmoja hadi mwingine ukifuata uzuri.

Kumpenda mtu bila kujua ni kwa nini umempenda, kuna maana ya kumkubali mtu huyo kama alivyo, kumpokea bila masharti. Kuna maelezo na nadharia nyingi zenye kuonyesha ni kwa nini siyo kila mtu anaweza kumpenda mwingine kwa njia hii.

Lakini bila shaka, nadharia na maelezo hayo hayana nafasi kubwa sana kwetu katika kujadili jambo hili. Chenye nafasi, ni kujua namna mtu anavyoweza kupima aina ya mapenzi aliyomo.


Share.

Leave A Reply