Wednesday, August 21

Waziri Mkuchika awataka Watumishi wa Wizara ya Madini kuwa Wazalendo

0


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu George Mkuchika amewata Viongozi na Watumishi wa Wizara ya Madini na Taasisi zake kuwa wazalendo ili kuifanya Sekta ya Madini   kuifikisha  nchi  katika uchumi wa Kati ifikapo mwaka 2025.

Kapteni Mkuchika amesema Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2025 Ibara ya 35 ni kuifanya sekta ya madini kukua na kuongeza mchango wake kwenye pato la taifa.

Ameyasema hayo, wakati akifungua mafunzo ya siku Nne ya Viongozi wa Wizara na Taasisi zake pamoja na Maafisa Madini Wakazi kutoka mikoa yote nchini inayofanyika katika Ukumbi wa St.Gasper, Jijini Dodoma.

Mkuchika ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais John Magufuli kwa kusimamia Ilani ya Chama Cha Mapunduzi na kutekeleza ahadi kwa kuchukua hatua mbalimbali katika kuboresha sekta ya madini.

Akielezea hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano amesema ni pamoja na kuanzishwa kwa wizara ya mahususi ya madini, kutunga Sheria Mpya ya Usimamizi wa Madini, Kuunda Tume ya Madini, Kusimamia mifumo na maboresho kadhaa  katika sekta ya madini na kukiri kuwa, hatua hizo zinaonesha  dhamira ya Serikali kuifanya sekta ya madini kuchangia zaidi pato la Taifa.

Aidha, amesisitiza kuwa, ili Serikali iweze kufikia malengo yake, kila mmoja anapaswa kutanguliza uzalendo mbele katika kudhibiti vitendo vya kuhujumu jitihada za serikali vya kupambana na wizi na ubadhirifu katika sekta ya madini na sekta nyingine.

Vilevile, amewataka viongozi hao kuielewa na kusimamia Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma, Sheria ya Utumishi wa Umma, Kanuni pamoja na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali lengo likiwa ni kuleta ufanisi wa hali ya juu katika utendaji unaozingatia sifa, weledi na maadili.

Pia, Waziri Mkuchika amekiri kufurahishwa na ushiriki wa viongozi wa Makao Makuu ya Wizara na taasisi zake katika mafunzo hayo na kuwataka kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu mafunzo hayo ikiwemo kuuliza maswali ili kupata ufafanuzi na uelewa  ili yawezeshe kuleta tija kwa wizara na taasisi zake.


Share.

Leave A Reply