Monday, June 24

Upinzani watoa msimamo mkali suala la Mahakama kutengua Wakurugenzi kusimamia uchaguzi

0


Sisi viongozi waandamizi wa vyama vya ACT Wazalendo, CCK, CHAUMMA, CHADEMA, DP, NCCR Mageuzi, NLD na UPDP tumeipokea, kuipitia kwa kina na kuichambua hukumu ya kihistoria iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam kwenye shauri la kikatiba Namba 17 la mwaka 2018 (Bob Chacha Wangwe Vs The Attorney General and Two Others).

Kabla ya kutoa msimamo wetu kama wadau muhimu kwenye hukumu hiyo, tunapenda kwanza kutoa pongezi kwa Mwanaharakati Bob Chacha Wangwe na wakili wake Fatma Karume kwa kufungua na kuisimamia kesi hiyo ambayo imezaa maamuzi ya kihistoria yaliyotolewa na Mahakama Kuu chini ya Jopo la Majaji Mh. A. F. Ngwala, F. N. Matogolo na B.S Masoud.

Ushindi huu wa kihistoria umeonesha waziwazi umuhimu wa ushirikiano mpana (grand coalition) baina ya asasi za kiraia, wanaharakati, vyama vya kisiasa na wananchi kwa ujumla wake na jinsi unavyoweza kuimarisha, kuitetea na kuilinda misingi ya demokrasia nchini Tanzania.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 ipo wazi kabisa (Ibara ya 74(14) kwamba wasimamizi wa uchaguzi wasijihusishe na masuala ya vyama vya siasa. Kinyume na matakwa haya ya kikatiba, Wakurugenzi wa Halmashauri za Miji, Wilaya, Manispaa na Majiji wakitekeleza majukumu yao ya kusimamia uchaguzi wamekuwa wakiegemea waziwazi upande wa Chama cha Mapinduzi (CCM)

Chaguzi ndogo za marudio za hivi karibuni zinaweza kutoa mifano hai ya karibuni ya jinsi ya Wakurugenzi hawa ambao pia wengi wao ni makada wa CCM wanavyokipendelea waziwazi chama chao.

Mathalani, Jimboni Kinondoni kwenye uchaguzi wa marudio, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Mh. Aaron Kagurumjuli alikataa kutoa nakala za viapo vya mawakala kwa wakati. Uamuzi huu wa Mkurugenzi huyu ndio uliopelekea kifo cha mwanafunzi Akwelina.

Mfano mwingine ni wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Dk. George Nyaronga. Kwenye uchaguzi wa marudio katika jimbo la Korogwe vijijini kufuatia kifo cha Mh. Stephen Ngonyani (Dk. Maji Marefu), msimamizi huyo wa uchaguzi alitoweka ofisini kutwa nzima na kuibuka baada ya muda wa kupokea fomu kuisha na kumtangaza mgombea wa CCM Mh. Timotheo Mzava kupita bila kupingwa. Mifano kama hii ipo pia takribani kwenye chaguzi zote za nyuma.

Sisi viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani tunasema kwamba katika mazingira haya ya Wakurugenzi wanaokwepa kupokea fomu, wanaowaengua wagombea wa upinzani bila sababu za msingi na wanaofanya vitendo mbalimbali vya dhahiri vya kukipendelea Chama cha Mapinduzi, uamuzi huu wa Mahakama Kuu umekuja katika wakati muafaka na unapaswa kupongezwa.

Hivyobasi, tunaunga mkono maamuzi haya ya kutengua vifungu vya 7(1) na 7(3) vya Sheria ya Sheria ya Uchaguzi ambavyo vilikuwa vikiwapa madaraka Wakurugenzi kuwa wasimamizi wa uchaguzi.

Kama alivyokaririwa Jaji Mkuu Mstaafu Mh. Agustino Ramadhani ambaye amewahi kuwa pia Makamo Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, madai ya kutaka kuondolewa kwa Wakurugenzi ni matakwa ya muda mrefu ya wananchi. Sisi vyama vya siasa tumekuwa tukipaza sauti tangu miaka ya tisini kutaka wakurugenzi wasisimamie uchaguzi na kutaka tume huru ya uchaguzi kwa ujumla wake.

Pili, tunafahamu kwamba mapambano kwa ajili ya Tume Huru ya Uchaguzi yatafikiwa kwa kupata katiba mpya. Hivyo basi, sisi vyama vya siasa kwa kushirikiana na Asasi za Kiraia, wanaharakati, viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla tutaendelea kupigania katiba mpya itayoweka mazingira yenye usawa kwenye mfumo wetu wa uchaguzi utaosimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi.

Tangu Mahakama Kuu itoe maamuzi haya ya kihistoria, kumekuwepo na jitihada ndani ya serikali na CCM kujaribu kupotosha mantiki na msingi wa maamuzi haya. Kwenye tamko hili tungependa kuweka sawa baadhi ya upotoshaji huo.

1. Kuhusu Utekelezaji wa Hukumu

Inajaribu kujengwa picha kupitia tamko la Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa kusudio la ofisi hiyo kuukatia rufaa uamuzi huu wa Mahakama Kuu linasitisha utekelezaji wa uamuzi huu wa Mahakama Kuu.

Msimamo wa kisheria wa maamuzi haya ya Mahakama Kuu upo wazi kuwa vifungu vya 7(1) na 7(3) vya Sheria ya Uchaguzi ni batili kwa sababu ni kinyume na katiba. Hii ina maana kwamba kuanzia siku hukumu hii ilipotamkwa na Mahakama Kuu wakurugenzi ni MARUFUKU kusimamia uchaguzi hadi pale labda uamuzi huu utapotenguliwa na Mahakama ya Rufaa.

2. Kuhusu Sharti la Ibara ya 74 (14) ya Katiba Kuwahusu Wakurugenzi Baada ya Uteuzi.

Hoja hii, licha ya kurudiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya hukumu, lakini kwenye hukumu husika Mahakama Kuu imeweka bayana kuwa Wakurugenzi ambao ni makada au mashabiki wa CCM, maslahi au mapenzi yao kwa CCM huwa hayakomi baada ya kuteuliwa kuwa Wakurugenzi. Hivyo basi, katika zama hizi za demokrasia ya vyama vingi, haifai kuwatumia wakurugenzi ambao ni makada wa CCM halafu tukajidanganya kuwa haki itatendeka.

3. Hoja kwamba kuna wapinzani wamewahi kutangazwa na Wakurugenzi  hawa wanaopingwa. Hoja hii inayoshabikiwa na CCM ni dhaifu sana. Kwetu sisi wapinzani, mtu hatangazwi kuwa mshindi wa ubunge au udiwani hadi watu wauawe, wapigwe mabomu, wakamatwe, wafungwe au wabambikiwe kesi. Katika uchaguzi unaosimamiwa na Wakurugenzi makada wa CCM mpinzani hatangazwi mshindi hadi mbinu zote za kuiba kura zitaposhindikana.

Katika kuhitimisha, tunapenda kurejea rai yetu kuwa kutokana na maamuzi haya yanayoilazimisha NEC kuwa na watendaji wake wa kusimamia uchaguzi, huu ni wakati muafaka kwa uchaguzi wa serikali za mitaa nao kusimamiwa na NEC.


Share.

Leave A Reply