Monday, August 26

Lazima vijana waelewe kujiunga JKT si uhakika wa ajira – Waziri Mwinyi

0


Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Hussein Mwinyi amelieleza Bunge kuwa programu ya mafunzo kwa vijana inayotolewa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), haiwahakikishii ajira katika taasisi hiyo bali inawaandaa kujitegemea na kujiajiri.

Waziri Mwinyi ameyabainisha hayo leo, bungeni, Dodoma alipokuwa akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum, Angelina Malembeka aliyehoji uwepo wa manung’uniko ya vijana kukosa ajira hasa upande wa jinsia ya kike katika wilaya za Kaskazini na huko Zanzibar.

“Lazima vijana waelewe kuwa sio ajira, kujiunga JKT ni kwenda kujifunza mafunzo ya kijeshi pamoja na stadi za kazi.Tunachukua takribani vijana elfu 20 kwa mwaka, vyombo vya ulinzi na usalama havina uwezo wa kuchukua wote hao katika ajira,”alisema Dk Mwinyi.

Akifafanua zaidi, Dk Mwinyi amesema kuwa jukumu la ugawaji wa nafasi hizo za mafunzo halipo chini ya Wizara yake bali ni suala ambalo lipo chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo imekuwa ikipanga idadi ya vijana wanaotakiwa kujiunga kwa kila wilaya.

Waziri Mwinyi ameeleza uchache wa jinsia ya kike wanaojiunga na JKT unatokana na uchache wao wakati wa usaili huku baadhi wakikosa sifa zinazohitajika.


Share.

Leave A Reply