Wednesday, August 21

KAMATI YA BUNGE YAKIPONGEZA CHUO CHA UTUMISHI WA UMMA KWA UTENDAJI MZURI NA UJENZI WA JENGO KATIKA KAMPASI YA TABORA

0


 Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Dkt. Henry Mambo akitoa taarifa ya utekelezaji ya majukumu ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tawi la Tabora kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa ilipokitembelea chuo hicho kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la chuo Kampasi ya Tabora.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe. Jason Rweikiza (Mb) akiongozwa na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Dkt. Henry Mambo (kushoto) kwenda kushuhudia jengo la chuo Tawi la Tabora lililojengwa kwa jitihada za chuo kwa kutumia fedha za ndani. 
 ******************************************************
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa imeipongeza Menejimenti ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kwa utendaji mzuri na ujenzi wa jengo katika tawi la Tabora ambalo litatumika  kutoa mafunzo ya kozi mbalimbali zinazotolewa na chuo hicho ikiwa ni pamoja na kuendesha shughuli za kiutawala za chuo kwa ajili ya maendeleo ya chuo. 
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe. Jason Rweikiza (Mb) kwa niaba ya Kamati wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kutembelea jengo lililojengwa katika kampasi ya Tabora ili kujiridhisha na maendeleo ya ujenzi.
Mhe. Rweikiza amesema chuo kinastahili pongezi za dhati kwa hatua ya ujenzi iliyofikiwa hadi kufikia hatua ya kuezeka kwa kutumia mapato ya ndani ya chuo. 
Aidha, Mhe. Rweikiza  ameiomba  Serikali kusaidia  fedha za ukamilishaji wa ujenzi wa jengo hilo lililopo Kampasi ya Tabora kwani kozi zinazotolewa na chuo hicho kwa watumishi wa umma na wananchi ni muhimu kwa maendeleo ya nchi. 
Akitoa ufafanuzi kuhusu ujenzi katika Kampasi hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora, Kapteni (Mstaafu) Mhe. George H. Mkuchika (Mb) amesema jengo lilipofikia ni kwa jitihada za chuo chenyewe, hivyo wizara wamekaa na kukubaliana kuelekeza nguvu katika ukamilishaji wa ujenzi wa jengo hilo. 
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Aggrey Mwanri amesema Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania ni chuo ambacho kimeishi kwa sura ya jina lake lenyewe hususani kwa jitihada zake kubwa za ujenzi wa jengo katika kampasi ya Tabora na kuongeza kuwa jitihada hizo zinaonesha kuwa mkoa na uongozi wa chuo unao uwezo wa kufanya makubwa ili kukiendeleza chuo cha Utumishi wa Umma. 
Awali, Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania Dkt. Henry Mambo akijibu swali kuhusu mpango wa chuo kufungua tawi makao makuu Dodoma, amesema kuwa chuo kina nyumba ambayo ni ndogo iliyopo mtaa wa Tabora na mwakani kimepanga kuifanyia ukarabati ili kianze kutoa kozi za muda mfupi. 
Dkt. Mambo ameongeza kuwa, Chuo kimepewa eneo la ekari moja ambalo halitoshi kwa ujenzi hivyo wameiomba Manispaa ya Dodoma kuwapatia ekari kumi (10) kwa ajili ya kuanza ujenzi wa chuo mjini Dodoma. 
Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) tawi la Tabora kipo katika eneo la ekari 15.3 ndani ya Manispaa ya Tabora. Menejimenti ya Chuo kwa kushirikiana na Wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora ipo katika hatua za mwisho za kupata Hatimiliki. 
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakiongozwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Jason Rweikiza (Mb) kushuhudia jengo la Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Tabora (linaloonekana) lililojengwa kupitia mapato ya ndani ya chuo.
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora, Kapteni (Mstaafu) Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akitoa ufafanuzi kuhusu ujenzi wa jengo la chuo Tawi Tabora kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa ilipoitembelea Kampasi hiyo kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Kampasi hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe. Jason Rweikiza (Mb) akitoa pongezi kwa Menejimenti ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kwa ujenzi wa jengo la chuo katika Kampasi ya Tabora.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Aggrey Mwanri akiishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa kukitembelea Chuo cha Utumishi wa Umma Tawi la Tabora kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la chuo katika Kampasi ya Tabora.Read More

Share.

Comments are closed.