Friday, August 23

WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUFANYA KAZI ZAO KWA WELEDI

0


WAANDISHI wa habari wametakiwa kufanya kazi zao kwa weledi na kusaka vyanzo tofauti katika habari zao badala ya kuegemea chanzo kimoja.

Hayo yalielezwa jana katika uzinduzi wa machapisho ya matatu ya Baraza la Habari Tanzania (MCT), ambayo ni ripoiti ya hali ya tasnia ya habari nchini ya mwaka 2017/2018 iliyoandikwa na Dr. Joyce Bazira, Muhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar Dr Ali Uki na Henry Muhanika, chapisho la pili ni ukiukwaji wa maadili kwenye tasnia ya uandishi wa habari kilichoandikwa na Mhariri wa Gazeti la Daily News Pudenciana Temba na Attilio Tagalile, wakati chapisho la tatu ni fani ya uwandishi katika habari za kiuchunguzi zinavyoathirika ikitolea mfano kesi ya waandishi wa habari Ruvuma , ambapo kimeandikwa na Hamis Mzee, Lucas Liganga na Florence Majani.

Katika utafiti huo wa MCT unaonyesha kuwa vyombo vingi vya habari nchini vinakabiliwa na ugonjwa wa chanzo kimoja cha habari (SSS).

Akisoma ripoti hiyo, Mwenyekiti mstaafu wa Jukwaa la Wahariri Absalom Kibanda alisema kinachosikitisha zaidi kuhusu chanzo kimoja cha habari ni kwamba hutawaliwa na sauti za wanaume.

“Utafiti mmoja mahususi uliofanywa na MCT umeonyesha gazeti la Mwananchi lilikuwa na habari 99 za chanzo kimoja, ya vyanzo viwili zilikuwa 63 na habari za vyanzo vingi zilikuwa 158, habari zenye sauti za wanaume 1,913 sawa na asilimia 95 wakati zenye sauti za wanawake ni 93 sawa na asilimia tano.

Alisema utafiti huo pia umeonyesha gazeti la Nipashe lilikuwa na habari za chanzo kimoja ni 184, zenye vyanzo viwili ni 133 na habari za vyanzo vingi ni 103, habari zenye sauti za wanaume 1,307 sawa na asilimia 94 na zenye sauti za wanawake zilikuwa 88 sawa na asilimia sita wakati gazeti la Uhuru lilikuwa na habari za chanzo viwili zilikuwa 155 na habari za vyanzo vingi zilikuwa 204, huku zenye sauti za wanaume 3,111 sawa na asilimia 95 wakati sauti za wanawake zilikuwa 237 sawa na asilimia nane.

“Takwimu hizo zinaonyesha ukubwa wa tatizo ambalo lazima lishugulikiwe haraka na vyombo vya habari vya ndani, mfano kuna wakati Zito Kabwe anageuzwa yeye ndio waziri wa fedha, ndio profesa wa uchumi, ndio CAG, mchambuzi wa mambo ya uchumi, habari ukiikuta ni Zito alisema, aliongeza, alifafanua, waandishi toeni haki ya kujibu, hii itasaidia kukwepa vitanzi vya kisheria.”alisema Kibanda na kuongeza

“The Citizen walifungiwa wiki mbili, mimi namuunga mkono Dr Abbas kwa vile waliegemea upande mmoja walipaswa kupata upande wa pili lakini walikuwa na haraka, juzi kuna vyombi vya habaru vimeandikiwa barua baada ya kuandika ripoti aliyotoa Zito, ni sahihi kwa vile hawakutoa haki kwa mamlaka nyingine kujibu, hii ingesaidia, wasingepata kitanzi cha kisheria.”alisema Kibanda

Alisema changamoto kubwa kwa sasa hali ya uandishi wa habari ina wasomi lakini kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa kimaadili, msingi ya kitaaluma leo hii kuliko miaka ya nyuma ambapo wasomi walikuwa wachache.

“Waandishi wanatakiwa kujitazama na kujitathmini kama wanatimiza wajibu wao kitaaluma, mnapaswa kuwa makini kuliko wakati mwingine wowote.”alisema na kutolea mfano waandishi wa mitandao ya kijamii hususani you tube ambayo wamekuwa wakitoa kipande kidogo kwa makusudi na kuharibu maana nzima ya habari.

Akitolea mfano online tv alisema misingi ya kitaaluma inabidi ielekezwe huko kwani wamekuwa wakipotosha zaidi, bila kujali usahihi ulivyo na kusababisha mkanganyiko kwa jamii.

“Usahihi ni msingi namba moja hasa kwenye mitandao ya kijamii ambayo inafatiliwa kwa haraka, Uhuru uliopo usipitilize, misingi, maadili na miiko ya taaaluma inabidi itimizwe, la sivyo tusipotimiza hili, tutakwisha.”alisema

Alisema waandishi wa mitandao ya kijamii wanapaswa kufuata msingi wa kutoegemea upande wowote, na kuzingatia misingi ya kutoa haki na wajibu.

Kwa upande wa gwiji la habari, Pili Mtambalike ambaye alifanya rejea ya chapisho la Ukiukwaji wa Maadili kwenye Tasnia ya Uandishi wa Habari alisema ripoti hiyo imechukua miaka miwili ambayo ni 2017 na 2018 ambayo imepitia masuala ya sheria, sera, kanuni na changamoto mbali mbali zinazotokana na sheria za vyombo vya habari, kanuni na athari zitokanazo na sheria mpya ya vyombo vya habari.

Naye Atilio Tagalile akizungumzia ripoti ya Ruvuma ambayo waandishi wameenda kinyume na maadili ya vyombo vya habari alisema waandishi wanapaswa kushikamana na sio kuumizana na wasikubali kutumika.

“Waandishi wengi wa sasa ni wasomi, lakini inasikitisha baadhi yao hawana weledi kwenye kazi yao, nawakumbusha kwa nyakati hizi mnapaswa kufanya kazi zenu kwa umakini na weledi wa hali ya juu, la sivyo kuna anguko zaidi katika tasnia ya uandishi iwapo hatua hazitachukuliwa haraka.”alisema

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga alisema hali ya uhuru wa vyombo vya habari nchini imeporomoka kwa nafasi 47 katika nchi ndani ya miaka mitatu kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka 2018, ambapo mwaka 2016 iliporomoka nafasi 12, mwaka 2017 ikaporomoka nafasi 10 na mwaka 2018 imeporomoka nafasi 25.

Share.

Leave A Reply