Saturday, August 24

RAIS DK. MAGUFULI AAGIZA KUCHUKLIWA HATUA WAFANYABIASHARA WANAOPANDISHA BEI ZA VYAKULA KATIKA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHAN

0


Ikulu, Dar es Salaam
Rais Dkt. John Magufuli, pamoja na kuwatakia heri ya mfungo wa Mwezi mtukufu wa Ramadhani amezitaka Mamlaka za Serikali kuchukua hatua dhidi ya wafanyabiashara wenye tabia ya kupandisha bei za vyakula wakati wa Mfungo wa Mwezi huo.

Rais Magufuli ametoa kauli hizo leo wakati akihutubia katika Mashindano Maalum ya 20 ya Qur’aan Tukufu Afrika yaliyohusisha washiriki kutoka nchi 18 za Afrika na kufanyika katika Uwanja Mkubwa wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

Ameipongeza Taasisi ya Al-Hikma kwa kuandaa mashindano ya Qur’aan Tukufu yaliyojumuisha nchi mbalimbali za Afrika, na kwa kushirikiana na Serikali katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii.

Rais Magufuli amesema pamoja na kujenga Misikiti 50 hapa nchini, Serikali inatambua kuwa Taasisi ya Al-Hikma imesaidia jamii kwa kuchimba visima vya maji 110, kujenga shule moja ya msingi na shule mbili za Sekondari na inawasomesha watoto yatima 400.

Kutokana na mchango huo, Rais Magufuli ameishukuru taasisi hiyo pamoja na taasisi zingine mbalimbali zinazomilikiwa na Madhehebu ya Dini ambazo zimekuwa zikitoa mchango mkubwa katika kuhudumia jamii kwenye sekta za elimu, afya na kutoa misaada ya kibinadamu.

Kufuatia maombi yaliyotolewa na Taasisi ya Al-Hikma, Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo kuhakikisha taasisi hiyo inapatiwa hati ya umiliki wa eneo ililoomba libadilishiwe matumizi kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya kitakachotoa huduma kwa wananchi wote ifikapo Ijumaa (24 Mei, 2019).

Aidha, Rais Magufuli amewapongeza washiriki wote wa mashindano hayo ya Qur’aan Tukufu, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Serikali ya Saudi Arabia na wadau mbalimbali kwa kufanikisha mashindano hayo ambayo licha ya kuimarisha misingi ya kumcha Mwenyezi Mungu, yanaimarisha uhusiano baina ya Tanzania na Saudia Arabia pamoja na Mataifa yote yanayoshiriki.

Amemuomba Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wa Saudi Arabia Dk. Swalehe Al-Sheikh (ambaye amehudhuria katika mashindano hayo) kufikisha salamu zake kwa Mfalme wa Saudi Arabia, ambapo pamoja na shukrani kwa uhusiano mzuri wa Tanzania na Saudia Arabia na kuiomba nchi hiyo kujenge Msikiti mkubwa hapa nchini kwa ajili ya Waislamu kufanya Ibada zao.

Rais Mstaafu Alhaji Dk. Ali Hassan Mwinyi amemshukuru Rais Magufuli kwa kuungana na Waislamu katika mashindano hayo na amewataka Watanzania kuendelea kumuombea kutokana na kazi nzuri anazozifanya za kusukuma mbele gurudumu la maendeleo kwa kasi kubwa na kudumisha umoja wa Watanzania.

Naye Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete amesema uwepo wa Rais Magufuli katika mashindano hayo na hotuba aliyoitoa imedhihirisha dhamira yake ya kuimarisha umoja na mshikamano kwa Watanzania wote na kwamba Waislamu wote wamefarijika sana.

Baadaye Rais Magufuli alikabidhi zawadi kwa washindi wa mashindano hayo ambapo aliyeibuka mshindi wa kwanza ni Mouhamed Diallo (Senegal), wa pili ni Faruq Kabiru Yakubu (Nigeria), wa tatu ni Shamsuddin Hussein Ally (Zanzibar), wa nne ni Idrissa Ousmane (Niger) na wa tano ni Sumaiya Juma Abdallah (Pwani, Tanzania). 

Pamoja na viongozi hao, mashindano hayo yamehudhuriwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma, Makamu wa Rais Mstaafu Dk. Mohamed Gharib Bilal, Mawaziri, Mabalozi wa nchi mbalimbali na viongozi mbalimbali wa Madhehebu ya Dini na vyama vya siasa. Picha tele za Mashindano hayo/BOFYA HAPA

from CCM Blog http://bit.ly/30rL1TT
via

logoblog

Thanks for reading RAIS DK. MAGUFULI AAGIZA KUCHUKLIWA HATUA WAFANYABIASHARA WANAOPANDISHA BEI ZA VYAKULA KATIKA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHAN

Share.

Leave A Reply