Tuesday, August 20

RAFIKI YANGU WA MUDA MFUKO RAMBO REST IN PEACE,SITAKUHTAJI TENA

0


Na Said Mwishehe,Globu ya jamii 

SIKUMBUKI ni lini kwa mara ya kwanza Mfuko wa Plastiki maarufu kwa mfuko wa Rambo uliingia nchini.Sikumbuki. Ndio. 

Ila ninachokumbuka mfuko wa Rambo kwa hapa nchini umeishi kwa muda mrefu sana.Kuna watu tunao hapa nchni wamezidiwa umri na mfuko wa Rambo. 

Na kwa sehemu kubwa watu wamekuwa wakiitumia kubebea bidhaa mbalimbali.Wapo waliokuwa wanaitumia kubebea vyakula, wapo waliokuwa wanaitumia kubebea nafaka na wapo waliokuwa wanaitumia kwa matumizi mbalimbali. 

Ama kweli mfuko wa Rambo ulikuwa rafiki wa kila mtu.Hukuwa mbishi kwani kila aliyehitaji kukutumia alikupata.Kwa umri wako hapa nchini Tanzania wengi wamekutumia.Walikuamini kwani hukuwa mrahisi rahisi.Wewe mfuko wa Rambo ulikuwa mgumu tena mgumu haswaa .Ngoja nitumie lugha rahisi mfuko wa Rambo ulikuwa imara sana. 

Wakati unaingia nchini mfuko wa Rambo umaarufu wako ulishika kasi kama moto wa kifuu.Unajua kwanini jina lako la Rambo ni jina maarufu kwani kabla ya hapo tayari wengi wetu tulikuwa tunalisikia na kuliona kwenye filamu za mapigano. 

Kuna jamaa anaitwa Sylvester Stallone a.k.a Rambo.Huyu ni jamaa hajawahi kuja nchini Tanzania lakini maarufu sana.Filamu zake nyingi zimepata nafasi ya kutamba katika nchi yetu.Nusu ya kizazi cha Watanzania kimewahi kutazama au kusikia uwezo wa Rambo. 

Katika mabanda ya kuonesha video miaka ile ya nyuma nyuma , haipiti wiki bila kuoneshwa picha la Rambo.Ndio maana mfuko wa plastiki uliokuwa na picha ya Rambo aliyevalia kitambaa cha usongo kichwani ikapata umaarufu. 

Kuanzia hapo kila mtu akienda kununua bidhaa hataki tena kubeba kikapu kisa kuna mfuko wa Rambo.Kila mahali Rambo…yaani Rambo Ramboo.Mitaani huko mifuko ya Rambo ikawa inazagaa.Ni kweli kwa wakati ule wengi wetu tuliamua tu kutaza faida ya mfuko wa Rambo katika kubebea vitu mbalimbali. 

Hatukuwahi kuwaza madhara yake.Kila mmoja aliamini mfuko wa Rambo poa tu, Mbona freshi yaani kama naweza kubebea machungwa au ndizi zikafika nyumbani salama tatizo liko wapi? Maskini ya Mungu hatukuwa tunajua madhara yake. 

Uwepo wa mifuko ya plastiki ukiwemo huo wa Rambo madhara yake ni makubwa.Tena makubwa sana na hasa katika eneo la kimazingira.Ni mifuko ambayo imesababisha madhara makubwa ndani ya jamii yetu.Mifugo mingi imekufa kwasababu tu ya kula plastiki.Mitaro ya kupitisha maji taka nayo mingi imeziba kisa mifuko ya plastiki. 

Binafsi nikiri nilikuwa na urafiki mkubwa na mifuko ya plastiki lakini baada ya Serikali yangu ya Awamu ya Tano kuamua kueleza madhara yake kwa kweli sitakaa niitumie tena. 

Kwani kuna ubaya gani unapoamua kumuweka kando rafiki ambaye uliamini ni msaada kumbe ana madhara makubwa katika maisha yako na kama si yako basi ya anayekuja.Potelea mbali sitaki tena urafiki na mifuko ya plastiki. 

Nitatafuta mfuko mbadala wa kubebea bidhaa zangu.Samahani kama nitakuwa nimekukwaza unayesoma hii kitu.Naomba tu niseme huko unakokwenda mfuko wa plastiki nenda ukapumzike kwa amani(RIP mfuko Rambo). 

Kwa mujibu wa watalaamu na wanamazingira wanaeleza wazi mfuko wa plastiki unapotengenezwa unakaa kwa miaka 500.Yaani chukulia mfuko wa plastiki ambao umetengenezwa mwaka huu 2019, utakuwepo duniani kwa muda gani. 

Mimi, wewe na atakayezalizwa miaka 100 ijayo ataukuta na ataucha.Basi bora ungekuwa hauna madhara.Ukweli madhara ni makubwa makubwa sana. Kwanza nikumbushe tu, kesho ni marufuku kuzalisha, kutumia, kuuza au kununua mfuko wa plastiki.Ukiona unaupenda sana basi mwisho wako iwe leo.Ndio leo ndio mwisho. 

Serikali kupitia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa imetoa katazo la kisheria kwamba kunzia Juni 1,2019 mifuko ya plastiki ni marufuku kuonekana mtaaani, majumbani, viwandani na maeneo yote ya shughuli za kiuchumi.Wafanyabiashara wa Kariakoo jijini Dar es Salam mmeishi na mfuko wa Rambo na ule uliopewa jina la Kariakoo kwa muda mrefu. 

Iwe mwisho …sio nakuja kununua bidhaa unanipa mfuko wa plastiki sitakuelewa.Na nitakuwa mnoko kweli, nikiuona tu nakuchongea kwa wenye mamlaka. 

Watanzania wote tuunge mkono jitihada hizi za Serikali za kukomesha mifuko ya plastiki.Tena nikung’ate sikio Tanzania sio wakwanza kwani nchi zaidi ya 127 duniani zimepiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki.Yaani tunakoelekea tunakwenda pazuri sana.Natamani kutumia ule msemo wa SISI TANZANIA MPYA…TUKO VIZURI ila naogopa maana unawenyewe.Tukatae kutumia mifuko ya plastiki. 

Wanaokubaliana nami tuwasiliane:0713833822 

from MICHUZI BLOG http://bit.ly/2QAh4g0
via

logoblog

Thanks for reading RAFIKI YANGU WA MUDA MFUKO RAMBO REST IN PEACE,SITAKUHTAJI TENA

Share.

Leave A Reply