Monday, August 26

MKURUGENZI MTENDAJI TASAF AWAFUNDA VIONGOZI WA PEMBA KUHUSU SHUGHULI ZA TASAF.

0


NA. Estom Sanga-Pemba 

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF- Bwana Ladislaus Mwamanga, ametoa wito kwa viongozi wa serikali kisiwani Pemba kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na Mfuko huo ili iendelee kutoa tija kwa wananchi. 

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TASAF ametoa rai hiyo alipofungua kikao kazi kilichojumuisha wakuu wa mikoa, wilaya, Maafisa Wadhamini ,makatibu tawala na waratibu walioko kisiwani Pemba ambao pamoja na mambo mengine walipewa fursa ya kujadili utekelezaji wa miradi ya ajira ya muda na namna ya kusimamia na kutunza vifaa vya utekeleza ji wa miradi hiyo. 

Bwana Mwamanga amesema serikali kupitia TASAF imekuwa ikitekeleza miradi ya ajira ya muda kwa lengo la kuwaongezea walengwa wake kipato na kupunguza kero zinazowakabili, kazi inayoambatana na ununuzi wa vifaa ambavyo amesema vinatakiwa kutunzwa ili viweze kudumu na kukidhi matakwa ya wananchi. 

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TASAF amebainisha kuwa dhamira ya serikali ya kuwapunguzia wananchi adha ya umaskini kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini imepewa msukumo mkubwa zaidi na serikali na hivyo kuwataka viongozi wa ngazi zote kwenye maeneo yao kuwa karibu zaidi na miradi inayotekelezwa kupitia Mpango huo unaohudumia zaidi ya Kaya Milioni Moja na Laki Moja kote Tanzania Bara, Unguja na Pemba. 

Aidha Bwana Mwamanga amewajulisha viongozi hao kuwa Serikali imekamilisha maandalizi ya utekelezaji wa sehemu ya pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambao mkazo mkubwa utawekwa katika kuwashirikisha Walengwa wenye uwezo wa kufanyakazi kwenye miradi ya Maendeleo na kisha kulipwa ujira ili waweze kujiongezea kipato. 

Kwa upande wao viongozi hao wa Kisiwa cha Pemba walipongeza hatua ya serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambao wamesema umeleta matumaini kwa wnaanchi ambao walikuwa wanaishi kwenye hali ya umaskini mkubwa. 

Wamesema serikali kupitia TASAF imeamusha ari ya wananchi hususani walengwa kujiletea maendeleo kwa kuanzisha miradi ya uzalishaji mali na hivyo wakashauri idadi kubwa zaidi ya wananchi wanaoishi kwenye umaskini uliokithiri ijumuishwe kwenye mpango huo ili pia waweze kunufaika na huduma zake.

Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Bw. Ladislaus Mwamanga (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Pemba baada ya ufunguzi wa kikao kazi cha viongozi hao kilichofanyika kisiwani Pemba. 

Baadhi ya viongozi kisiwani Pemba wakiwa kwenye kikao kazi kilichojadili masuala mbalimbali yakiwemo wajibu wa viongozi katika kusimamia miradi na vifaa vya TASAF.Kikao kazi hicho kilifanyika kisiwani Pemba.

Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bw. Ladislaus Mwamanga (aliyesimama) akifungua kikao kazi cha viongozi wa Pemba waliojadili utekelezaji wa shughuli za TASAF kisiwani humo.

from MICHUZI BLOG http://bit.ly/2WwmMoq
via

logoblog

Thanks for reading MKURUGENZI MTENDAJI TASAF AWAFUNDA VIONGOZI WA PEMBA KUHUSU SHUGHULI ZA TASAF.

Share.

Leave A Reply