Monday, June 17

RC MAGANGA ATOA AGIZO KWA WAKUU WA WILAYA NA WAHANDISI KIBONDO NA KAKONKO

0


Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga amewaagiza wakuu wa wilaya za Kibondo na Kakonko pamoja na wahandisi wa wilaya hizo kuweka kambi katika kata ya Muhange kuhakikisha wanasimamia kwa pamoja mradi wa maji wa Muhange unatoa maji kwa wananchi ndani ya wiki mbili.

Kauli hiyo ameitoa wakati akiwa katika ziara ya kikazi kukagua maendeleo ya miradi ya maji ndani ya wilaya ya Kakonko ambapo alisikitishwa na kitendo cha mradi wa maji Muhange kutokamilika licha ya kwamba ulianza kutekelezwa tangu mwaka 2012 kwa ufadhili wa Benki ya dunia na ulitarajiwa kukamilika Desemba 2013.
Brigedia Maganga alisema ni jambo la kushangaza kuona wananchi wanaendelea kupata shida ya maji huku mradi ukiwa umefungwa kwa changamoto ndogo ndogo ambazo zinaweza kufanyiwa marekebisho na ukizingatia mradi huo unasimamiwa na wilaya mbili na wahandisi wawili hivyo aliwataka kutenga muda wa siku mbili kufika katika kijiji cha Muhange kushirikiana na wananchi kukamilisha mapungufu ya mradi huo. 
“Ukiwa kama Mhandisi kazi yako ni kukaa sehemu ya mradi hadi mradi utakapokamilika, kama mngekuja kukaa hapa changamoto hizi zisingejitokeza.. mmewaachia wakandarasi wafanye mradi kwa kiwango cha chini.. wananchi wanapampu maji yanaishia chini na hayawafikii na wananchi wanaendelea kuteseka”, alisema Brigedia Maganga.
“Wakuu wote wa wilaya mbili kaeni na hii kamati ya watumia maji na wataalamu wenu mje hapa na Jumuiya ya watumia maji kama tatizo la mabomba mtafute maeneo yanayovuja yafanyiwe ukarabati kama kuna tatizo la kisiasa litajulikana… suala ni kwenye utendaji na utekelezaji mpaka maji yaende kwenye gati zote 24 wananchi wapate maji”, alieleza mkuu huyo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya kakonko Kanali Hosea Ndagala alipokea maelekezo hayo na kuahidi kwenda kukaa pamoja na viongozi hao na kujadili mbadala wa kufanya haraka ilikuweza kukamirisha lengo la serikali kufadhili miradi hiyo kwa wananchi .
Naye Mhandisi wa wilaya ya Kibondo Michael Nguruwe alisema mradi huo ulikuwa ukisimamiwa na wilaya hiyo na mradi ulikaguliwa ,baada ya kukamilika kwa mradi huo wakati wa kufanya majaribio mradi ulitoa maji kwa magati yote 24 na matatizo hayo yamejitokeza baada ya wananchi kuanza kutumia mradi huo.
Alisema mradi unapokuwa hautumiki kwa muda mrefu matanki yanakauka na miundombinu inaharibika hali hiyo inaweza kusababisha mabomba kupasuka na tanki kuanza kuvuja na aliomba wakae pamoja na wataalamu wa wilaya ya Kakonko kufanya marekebisho na kupita kila eneo ambalo linavuja.
Diwani wa kata ya Muhange Ibrahim Katunzi alisema ukweli ni kwamba maji wanapoyaruhusu kwenda kwa wananchi bomba zinapasuka, bomba zilizowekwa hazina ubora na wanapata hasara kwa kuwa maji yote yanaishia njiani na hayawafikii wananchi na kufanya jumuia ya watumia maji kushindwa kuendesha mradi huo.
Alisema kwenye chanzo kinachotakiwa kuruhusu maji kuingia kwenye tanki, tanki halina chujio hivyo tope na vyura vinajaa kwenye tanki na hivyo kusababisha maji kusukumwa kwa kasi ndogo hali iliyopelekea wananchi wa kata hiyo kuukataa mradi huo.
Nao baadhi ya wananchi wa Vijiji vya muhange ya juu na chini Simoni Matulane na Anitha Ntibagomba walisema wananchi wanapata shida sana kufuata maji wengine wanaamka saa kumi na moja alfajiri na kufuata maji baadhi mpaka wanaingilia mito iliyoko mipakani kwa ajili ya kufuata maji.
Waliiomba serikali kuwasaidia wananchi kukamilisha mradi huo na utakapo kamilika wananchi wataendelea kuchangia na kuendesha miradi hiyo kama inavyoelezwa.
Mkuu wa mkoa wa Kigoma pamoja na Mradi huo alitembelea miradi miwili ya Nyagwijima na Gwanumpu ambapo katika miradi hiyo yote alibaini baadhi ya mapungufu na kuahidi kupeleka mafuta katika mradi wa Nyagwijima kupampu maji na kuhakikisha kama maji yanawafikia wananchi na wataalamu wanatakiwa kurejebisha miradi hiyo wananchi waanze kupata huduma.
Na Rhoda Ezekiel – Malunde1 blog
Mkuu wa mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga (katikati) kushoto ni Muhandisi Michael Nguruwe kulia ni Muhandisi Elinatha Elisha wakimuonesha moja ya Tanki la maji katika kata ya Nyagwijima wilayani Kakonko Mkoani Kigoma leo – Picha zote na Rhoda Ezekiel – Malunde1 blog

Read More

Share.

Comments are closed.